UKURASA WA 886; Watu Wanaokuzuia Kufanikiwa Lakini Huwajui Ni Hawa….

By | June 4, 2017

Pamoja na ugumu wa safari ya mafanikio, kutokana na vikwazo na changamoto ambazo tunakutana nazo, ipo pia changamoto kubwa ya watu wanaotuzuia tusifanikiwe.

Watu hawa wapo kwenye makundi mawili;

Kundi la kwanza ni wale wanaoweka wazi kabisa wanatupinga na kutuzuia kufanikiwa. Hawa wanatukatisha tamaa, kutuhujumu au kujaribu kutuzuia tusichukue hatua. Watu hawa ni rahisi kuwaona na kuwajua na hivyo tunaweza kuwakwepa.

Kundi la pili ni wale ambao hawaonekani wazi kama wanatuzuia. Hawa ni watu ambao wanafanya mambo yao, wala hata hawatupingi au kutuzuia tusifanye yetu. Hawa ni wale watu wa karibu sana kwetu, tunaofanya nao kazi na biashara zetu na hata tunaokuwa nao karibu muda mwingi. Watu hawa hawafanyi chochote kuonesha kwamba wanatupinga, ila uwepo wao kwenye maisha yetu ndiyo unakuwa na madhara kwetu.

SOMA; Tabia Saba (07) Za Watu Wenye Ufanisi Mkubwa, Na Wanaofanikiwa Sana.

Kwa kifupi ni kwamba, huwezi kufanikiwa zaidi ya wale ambao wanakuzunguka, huwezi kabisa, wala usijidanganye kwa hilo. Wazazi wetu enzi hizo waliona mbali kwenye malezi walipotuambia tusikae na watoto wenye tabia mbaya, maana na sisi tutakuwa na tabia mbaya. Huenda ulijaribu kuwaambia ni marafiki zangu tu, sitachukua tabia zao. Lakini huko ni kujidanganya.

Hata sasa hivi ukiwa mtu mzima kama ulivyo, bado utakuwa unaendelea kujidanganya kwamba marafiki zako na wale wanaokuzunguka wapo tu kwa urafiki, au kwa kazi. Lakini imedhibitishwa kwamba hawaishii kwenye kazi na urafiki tu, bali wanakuwa na madhara makubwa kwenye maisha yako yote. Kuanzia namna unavyofikiri, namna unavyofanya kazi zako, na hata mtizamo ambao unao kwenye maisha yako.

Watu hawa wa karibu yako hawatumii nguvu kubwa kukuzuia, bali wao wanaishi maisha yao, na wewe unajikuta unashawishika kuishi maisha ya ngazi zile zile. Na hapo utapata matokeo sawa na wao wanayopata. Kama unabisha hili, jaribu kuwaangalia wale watu wa karibu sana kwako, na uone kama mna tofautiana sana.

Hivyo rafiki, jukumu lako kubwa ni kuangalia watu gani wanaokuzunguka, watu gani ambao unatumia nao muda wako mwingi. Angalia wanaenda wapi, maana huko ndiyo na wewe utaenda. Pia angalia wanafanyaje, maana ndivyo na wewe utafanya.

Kama wanaokuzunguka hawaendi unapotaka wewe, tafuta wengine wanaoenda unakotaka. Kama safari yako ni kwenda Tanga, ila ukajikuta umepanda basi la Morogoro, unafanya nini? Rahisi, unashuka na kupanda basi sahihi. Kukaa kwenye basi lisilo sahihi hakuifanyi safari kuwa sahihi.

Kuwa macho sana na watu hawa ambao ni kikwazo kikubwa lakini hawaonekani. Chunga sana ule mduara wako wa ndani, yaani wale watu wa karibu sana kwako, wana athari kubwa kwenye maisha yako. Chagua watu sahihi, na kama huwapati basi tengeneza watu sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.