UKURASA WA 887; Giza Haliwezi Kupona Hapa…

By | June 5, 2017

Dawa ya giza ni mwanga, hivyo tu, hakuna la ziada. Palipo na giza, ukipeleka mwanga, giza linapotea lenyewe kabisa, haliwezi kupambana na mwanga. Hutakuja kuona au kusikia mapambano ya giza na mwanga, mwanga unapofika, giza linapotea lenyewe, bila hata ya kuulizwa.

Kadhalika kwenye ujinga, dawa ya ujinga ni elimu na kujifunza. Kadiri unavyojifunza, ndivyo unavyouweka ujinga pembeni. Kadiri unavyojua, ndivyo ujinga unavyokimbia wenyewe. Huwezi kujifunza kitu kwa kina hasa, halafu ukawa mjinga kabisa kwenye kitu hicho. Elimu inapokuja, ujinga unajiweka pembeni, wenyewe, bila hata ya kulazimishwa.

Kitu chochote ulichonacho kwenye maisha, ambacho hukitaki au hukipendi, wala usipambane nacho, badala yake tafuta mbadala wake. Tafuta kile chenye nguvu kabisa kwenye kitu hicho, na hapo utakikimbiza kabisa. Kama ilivyo kwamba ukiwa na panya wanakusumbua, hata wawe wakubwa kiasi gani, ukitaka kupambana nao wewe mwenyewe wanaweza kukusumbua. Lakini ukileta paka, wataisha au watakimbia wao wenyewe.

SOMA; Giza Sio Kitu…. Hofu Sio Kitu…..

Ukiwa na njaa, hakuna namna unaweza kupambana na njaa yako zaidi ya kula. Unapopata chakula njaa inaondoka yenyewe. Unaweza kuituliza tu kwa mengine utakayofanya, lakini lazima ule chakula kuondokana na njaa yako kabisa.

Uzuri wa asili ni kwamba, kila kisicho kizuri, kisicho bora, kina upande wake wa pili ambao una nguvu kuliko ule ambao huutaki. Unachohitaji kufanya wewe ni kuangalia kipi hutaki na kipi kina nguvu ambacho kikifika tu usichotaka kinaondoka chenyewe. Kama ilivyo baridi na joto, joto linapokuja, baridi inapotea yenyewe.

Unapoweka juhudi, uzembe unaondoka wenyewe. Unapoweka kazi, umasikini unapotea wenyewe.

Kile usichotaka, angalia kipi kina nguvu zaidi yake na fanya hicho.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 887; Giza Haliwezi Kupona Hapa…

  1. Pingback: Jinsi Ya Kumjua Mpumbavu Na Kumwepuka Ili Kupunguza Matatizo Kwenye Maisha Yako. – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.