UKURASA WA 905; Kulalamikia Nguvu Ya Mvutano….

By | June 23, 2017

Kinachotuzuia sisi binadamu kuruka kama ndege, ni kwa sababu hatuna njia ya asili ya kuweza kuishinda nguvu ya mvutano ya dunia. Ndiyo maana ukiruka juu, lazima utashuka chini, kwa sababu dunia inakuvuta.

Hii pia ndiyo ilikuwa changamoto ya kutengeneza ndege ya kwanza kuruka angani. Ilikuwa lazima kuweza kutengeneza mfumo wa kuishinda nguvu ya mvutano, ili chombo kiweze kupaa angani.

Iwapo watu wangelalamikia nguvu ya mvutano bila ya kuchukua hatua yoyote, hakuna ndege ambayo ingekuja kutengenezwa. Kwa sababu hakuna kinachobadili nguvu hiyo ya mvutano. Hivyo njia pekee ilikuwa ni kuangalia namna gani ya kuzidi nguvu hii ya mvutano, na kuweza kupaisha chombo. Nguvu haikuwekwa kwenye kuiondoa kabisa nguvu hii, kwa sababu hilo haliwezekani. Badala yake nguvu iliwekwa kwenye kutengeneza kifaa ambacho kitaizidi nguvu ya mvutano.

Hili ndilo tunalopaswa kufanya ili kufanikiwa.

SOMA; Njia Bora Kabisa Ya Kulalamika Ni Hii.

Kwa sababu zipo nguvu za mvutano ambazo zinatulazimisha kubaki pale ambapo tupo. Yapo mapungufu yetu wenyewe ambayo yanatuzuia kufanikiwa. Yapo mazingira na watu wanaotuzunguka ambao wanaweza kuwa kikwazo kwenye mafanikio yetu.

Hivyo jukumu letu kubwa, ni kuangalia namna ya kuvuka nguvu hizi. Badala ya kukazana kumaliza mapungufu yetu, tuangalie namna gani maeneo ambayo tupo vizuri yanaweza kutusogeza mbele zaidi. Badala ya kusubiri mpaka mazingira na kila mtu anayetuzunguka akubaliane na sisi, tuangalie namna gani tunaweza kutumia mazingira kama yalivyo kuweza kupiga hatua.

Kulalamika na kulaani kila kinachotuzuia hakutusaidii kwa namna yoyote ile kupiga hatua. Bali kuangalia kipi tunachoweza kufanya, kuvuka yale yanayotuzuia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.