UKURASA WA 907; Njia Nyingine Ya Kuishinda Hofu Ni Hii…

By | June 25, 2017

Kuielewa hofu, ni hatua muhimu sana ya kuweza kuishinda, isikuzuie kuchukua hatua ya mafanikio.

Kwa sababu kwenye kila jambo ambalo unataka kufanya, hasa linapokuwa jipya na kubwa, hofu hutawala.

Hofu hii inachangiwa na mengi, kwa kuanza na wewe binafsi, wanaokuzunguka na hata mazingira. Hii inatokana na ugeni wa jambo, mtazamo wa wengine na hata matokeo ya jambo hilo, iwapo litafanikiwa au litashindwa.

Wengi wanaopanga kufanya, huishia hatua hiyo ya mipango, wasiweze kuchukua hatua kwa sababu hofu huwazidi, nakuona ni vyema wakasubiri kwanza, labda mpaka watakapokuwa tayari, au mambo yatakapokuwa mazuri.

Ninachotaka uelewe rafiki, au ukumbuke maana huenda umesahau ni kwamba kila hofu ipo kwenye kila jambo ambalo tunapanga kufanya.

SOMA; Kilichojificha Nyuma Ya Hofu Ya Kufanya Mambo Makubwa….

Kwa kifupi ni kwamba hofu haitokani na jambo tunalotaka kufanya, bali mtazamo wetu binafsi juu ya jambo tunalotaka kufanya. Na kwa kuelewa hili, tunaweza kubadili mtazamo wetu, ili tuweze kuishinda hofu na kufanya.

Kwa mfano, kwa hali ya kawaida, huwezi kuruka ukuta mrefu, unahofia kuumia kama utafanya hivyo. Lakini iwapo utakuwa unafukuzwa na mbwa mkali, ambaye akikukamata atakuuma, ukikutana na ukuta utauruka bila hata kufikiri. Kwa sababu gani? Kwa sababu hofu ya kuumia kwenye kuruka ukuta, ni ndogo kuliko hofu ya kuumwa na mbwa. Hivyo mazingira yanabadili mtazamo ulionao juu ya hofu husika.

Kwa mfano huu, unaweza kubadili mazingira yoyote yanayokupa hofu ya kuchukua hatua, kwa kuweka hali ambayo itafanya kutokuchukua hatua kuwe na hofu kubwa kuliko kuchukua hatua.

Kama unataka kufanya jambo la kukuongezea kipato ila una hofu ya kushindwa, fikiria namna maisha yako yatakuwa magumu kama hutaongeza kipato chako sasa. Kadiri hofu hiyo inavyokuwa kubwa, utasukumwa kuchukua hatua.

Kumbuka, huwezi kuondoa kabisa hofu, bali unachoweza kufanya ni kuishinda. Tengeneza mazingira yatakayoishinda hofu ili uweze kuchukua hatua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.