UKURASA WA 915; Hivi Ndivyo Unavyotengeneza Siku Mbaya Kwako…

By | July 3, 2017

Unajiambia kwamba una siku mbaya, hivyo tu, wala hakuna muujiza.

Unapoianza siku, labda kwa changamoto fulani, kisha ukajiambia siku yangu imeshakuwa mbaya, basi utabiri wako lazima utimie. Siku hiyo lazima itakuwa mbaya sana, hata ufanye nini. Hii inatokana na ukweli kwamba kuanzia wakati huo, kila jambo utakalokutana nalo, utaona ubaya zaidi ya unavyoona uzuri wake.

Ukijiambia kwamba una siku nzuri, siku bora, hiyo ndiyo utakayoipata. Utakuwa na siku nzuri na bora, kila jambo linalotokea, utaangalia uzuri wake zaidi ya ubaya wake. Na hapo utaweza kufanya makubwa kwenye siku hiyo.

Hivyo rafiki, kuondokana kabisa na siku mbaya kwenye maisha yako, acha kujitengenezea siku mbaya. Acha kujishawishi kwamba siku yako ni mbaya. Hata ukutane na changamoto na vikwazo vikubwa kiasi gani, kumbuka ya kwamba hayo yote ni sehemu ya maisha, yatapita na maisha yataendelea tena.

SOMA; Uongo Huu Unaojiambia Kila Siku, Ni Adui Mkubwa Wa Mafanikio Yako.

Unapojitabiria una siku mbaya, unapokiri kwamba siku yako imeshaharibika, hakuna anayeweza kukushawishi tofauti na hapo. Na dunia itakuwa tayari kukuletea siku mbaya kama unavyotaka.

Kuna watu wanakutana na magumu na changamoto kubwa kila siku, lakini wanaonekana kusonga mbele kama vile hakuna kilichotokea, siri kubwa ni hii, hawakubali siku zao kuwa mbaya, wanafanya kile wanachoweza, na matokeo huwa yanakuwa bora.

Unapoianza siku yako rafiki, ianze kwa kukiri inakwenda kuwa siku bora, jiambie ni siku ya kipekee kwako. Na unapokutana na changamoto yoyote, kumbuka ni sehemu ndogo sana ya siku yako bora.

Hata kama unaumwa au umepatwa na msiba, bado hiyo ni siku bora kwako, kwa sababu yapo makubwa na muhimu unayojifunza kwenye maisha yako, ambayo ukiyatumia vizuri, utakuwa na maisha bora zaidi baada ya kupita kwa hayo.

Kubali kuwa na siku bora, na dunia haitakuwa na namna, bali kukupa wewe siku bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.