UKURASA WA 916; Usiitabiri Kesho Yako, Bali Itengeneze…

By | July 4, 2017

Katika kitu kimoja ambacho tunaongoza kwa kushindwa, ni utabiri. Sisi binadamu siyo wazuri kwenye utabiri wa aina yoyote ile. Hakuna mtu ambaye ameweza kuwa na utabiri wa uhakika wa asilimia 100. Mara nyingi wanaotabiri na ikatokea, inakuwa ni bahati pekee na wala siyo uhakika.

Pamoja na ubovu wetu huu kwenye utabiri, bado watu ambao hutabiri maisha yao ya kesho. Watu hufanya mambo kwa kutegemea labda kesho vitu fulani vitatokea na kuwawezesha kupata kile wanachotaka.

Hili siyo jambo la kutegemea, kwa sababu wengi wameangushwa kwa kutegemea mambo ambayo hawawezi kuyadhibiti kwa asilimia mia moja. Inakuwa ni kama mtu amejiandaa kushindwa, kwa sababu anategemea kitu ambacho hana uhakika nacho.

Njia bora ya kutengeneza kesho unayoitaka siyo kutabiri, badala yake ni kuitengeneza kesho yako. Hii ni njia ambayo wewe unaweza kuidhibiti na kuiathiri kadiri utakavyo.

SOMA; Maua Yatakayochanua Kesho…

Kwa mfano, upo hapo ulipo sasa, ukifanya hayo unayofanya sasa na kupata matokeo unayopata sasa, kwa sababu ya hatua ulizochukua jana na siku zilizopita. Kuna mambo ulifanya au hukufanya, ambayo yamechangia wewe kufika hapo ulipofika sasa.

Na hii ina maana kwamba kama unataka kuwa na kesho bora, basi lazima ufanye kitu leo ambacho kitaleta matunda mazuri kesho. Inaweza kuwa kujifunza mbinu na njia bora zaidi, au inaweza kuwa kujaribu kitu kipya, kuongeza ubunifu au kuwasiliana na mtu muhimu ambaye kwa ushirikiano wake, utaweza kufanya kwa ubora zaidi.

Badala ya kukaa na kutabiri, kwamba huenda kesho mambo yakawa mazuri, kwa nini usifanye kitu leo kitakacholeta matokeo tofauti kesho? Unaweza, chukua hatua sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.