UKURASA WA 946; Njia Bora Ya Kuzishinda Mashine Na Teknolojia Mpya…

By | August 3, 2017

Dunia imekuwa inapitia mapinduzi makubwa kila baada ya kipindi fulani. Palikuwepo na zama za mawe, zikaja zama za chuma, mapinduzi ya viwanda, zama za taarifa na sasa tunaingia zama za watu mashine. Huenda hujawahi kusikia hilo nililotaja mwanzo, na ni kwa sababu ni zama changa kabisa.

Sasa hivi juhudi kubwa zinafanyika kutengeneza mashine zinazofanya kazi kama watu kabisa, lengo likiwa kuchukua nafasi za watu kwenye maeneo mbalimbali. Siku hizi utakuwa umeona habari nyingi kuhusu maroboti yanayohudumia watu migahawani, yanayojibu simu na hata kuona magari yanayojiendesha yenyewe.

Kumekuwa na mwamko wa watu wanaotaka hilo lidhibitiwe kwa sababu litaathiri ajira za wengi. Wanaweza kuwa sahihi kabisa, lakini wanachosahau ni kwamba, huwezi kushindana na teknolojia, wakati wa jambo ukishafika umefika, huwezi kulizuia jambo ambalo wakati wake umefika.

Hivyo sehemu sahihi ya kuweka nguvu siyo kuzuia mashine zisichukue nafasi za watu za kazi, bali watu kuwa bora ili mashine zisiweze kuchukua nafasi zao. Naamini umenielewa hapo, unahitaji kuwa bora sana kiasi kwamba hata kama itakuja mashine bora kiasi gani, haitaweza kuondoa umuhimu wako kwenye kazi au biashara ambayo unaifanya.

Sasa, tofauti kubwa kabisa ya binadamu na mashine ni moja, binadamu ana utashi wa kufikiri, mashine haina. Mashine itaambiwa fanya A kisha B, halafu nenda C na kamalizie D. Mashine itataka ikute mtiririko huo, popote pakiwa tofauti, mashine inakwama. Ila mtu anaweza kubadili hali kulingana na mabadiliko yanayokuwa yametokea.

SOMA; Njia Bora Ya Kuwapima Wanaokuzunguka Kama Wanakufaa…

Changamoto kubwa sana ni kwamba, watu wengi wamegeuza ufanyaji wa kazi au biashara zao kuwa kama mashine. Wengi wanafanya kwa mazoea na wanafanya kitu kile kile kila siku. Kiasi kwamba ikigunduliwa mashine nzuri, watu hao hawana kazi. Kwa sababu mashine inaweza kuundishwa haraka sana kazi yoyote ua kujirudia na haina matatizo mengi.

Hivyo ili kuhakikisha mashine haiji kuondoa umuhimu wako, kuwa mbunifu, na ongeza thamani zaidi kwenye kile ambacho unafanya. Fanya kitu ambacho kitamshangaza yule ambaye anakipokea. Fanya kitu ambacho mtu anayekitegemea anasema hakika hichi ni kitu bora.

Hata kama umeajiriwa, ile kazi ambayo unachagua kuifanya, weka ubunifu wako ndani yake, weka utu wako ndani yake. Naweza kwenda mbali zaidi na kusema weka damu yako ndani yake.

Kadhalika kwenye biashara, wahudumie wateja wako kwa kiwango cha hali ya juu sana. Zungumza na wateja wako kama watu, na wewe kama mtu na siyo kuwachukulia kama idadi ya wanunuaji. Tatua changamoto zao, jua matatizo yao na nenda hatua ya ziada kuhakikisha wanapata huduma bora sana.

Usikae tu kwenye biashara kupokea fedha na kutoa bidhaa au huduma, bali kaa pale kama mtu ambaye umejitoa kutatua changamoto ya wengine, kutimiza mahitaji yao ya msingi.

Uzuri ni kwamba, ukianza kutekeleza hilo, wala siyo tu utaizidi mashine, bali utawazidi asilimia 90 ya wale wanaofanya kile unachofanya wewe. Kwa sababu wengi huwa wanafanya kwa mazoea, wanapenda kuweka juhudi kidogo wapate matokeo makubwa, sasa wewe unapochagua kwenda hatua ya ziada, unatoa thamani kubwa zaidi ya wale wanaofanya kwa kiasi pekee.

Huna haja ya kuhofia mashine wala ushindani, iwapo utajitoa kwenye chochote unachofanya. Jitoe kwa kuweka juhudi kubwa, kuweka ubunifu na kwenda hatua ya ziada kwa chochote unachogusa, na utakuwa mbali zaidi ya wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.