UKURASA WA 962; Dawa Kamili Ya Hofu Ya Kushindwa….

By | August 19, 2017

Kama kuna kitu ambacho kinawazuia watu wengi kufanikiwa basi ni hofu. Hofu imekuwa kikwazo kwa wengi kuchukua hatua na kuweza kufanikiwa kwenye maisha yao. Watu wanakuwa na ndoto kubwa, wanaweka mipango mizuri, lakini inapofikia kwenye utekelezaji, ndipo hofu huchukua hatua nafasi yake na watu hawaanzi.

Hofu zipo nyingi, lakini leo tunakwenda kuangalia hofu moja inayoongoza kwa kuua ndoto za watu wengi. Hofu hii ni hofu ya kushindwa. Hii imekuwa inawazuia wengi kuchukua hatua na kuweza kufanya makubwa. Kwa sababu kwa lolote kubwa ambalo mtu anapanga kufanya, ipo hatari ya kushindwa. Unapoanza kuangalia hatari hii, hofu inakupa sababu ya kwa nini usifanye. Vipi kama ukishindwa? Unaona hatari ni kubwa na kuacha.

Leo nakwenda kukushirikisha njia moja ya uhakika ya kuweza kuishinda hofu hii ya kushindwa. Lakini kabla ya hapo, kwanza tuangalie ukweli ambao wengi tumekuwa hatuoni kwenye aina yoyote ya hofu. Ukweli ni kwamba, mambo huwa hayawi mabaya kama tunavyofikiri yatakuwa. Hata kama mambo yatakwenda tofauti na tunavyofikiri, huwa hayawi mabaya kama tunavyokuwa tumefikiria yatakuwa. Huwa yanakuwa kwenye hali ya tofauti na tulivyotegemea, lakini maisha bado yanaendelea kwenda.

SOMA;  Usiendeshwe Na Hofu Kwenye Maamuzi Haya…

Zamani, enzi hizo wakati maisha yalikuwa ni hatari, kushindwa maana yake ilikuwa ni kifo. Lakini kwa zama tunazoishi sasa, ni mambo machache sana ambayo kushindwa kwako kutapelekea kifo. Na kama umeweza kusoma hapa, nina uhakika kwamba chochote utakachoshindwa, bado maisha yako yataweza kuendelea vizuri tu. Hivyo hofu yoyote tunayokuwa nayo, haina maana kwa sababu maisha yetu yanaweza kwenda vizuri kwa matokeo yoyote tunayoyapata.

Sasa kwenye dawa ya hofu ya kushindwa, kwa sababu hofu hii imekuwa inawapooza watu wasichukue hatua kabisa, licha ya kuwa na mawazo mazuri na ndoto kubwa.

Dawa ni kuanza kidogo, anza kidogo kabisa, kwa hatua ndogo sana ambayo hata ukishindwa hutajali au maisha yako hayatakuwa hatarini kama unavyohofia.

Kwa mfano, kama unachopanga ni kuanza biashara, lakini una hofu kubwa ya kuanza, labda unaona biashara hiyo inafanywa na kila mtu, au huna uhakika kama itafanya vizuri kama unavyotegemea, unaweza kuamua kuanza kidogo kabisa. Anza kwa kiasi ambacho hata ukipata hasara kabisa maisha yako hayatakuwa hatarini. Anza ukiwa na lengo la kujifunza na kuwa tayari kupoteza. Kisha anza na jifunze kadiri unavyokwenda.

Weka lengo dogo kabisa unaloweza kulifanyia kazi kwa siku moja, halafu mwisho wa siku jifanyie tathmini umeweza kulifanya kwa kiasi gani, wapi umefanya vizuri na wapi una changamoto. Kesho panga kupiga hatua nyingine ndogo na endelea kupiga hatua hivyo kila siku, baada ya muda utakuwa upo mbali sana ukilinganisha na kama usingeanza kabisa.

Kwa kuweka mipango midogo na kuifanyia kazi, unaiua hofu kabisa kwa sababu kwanza unajizoesha kufanya kile ambacho hujazoea kufanya, na unafanya hivyo kwa ngazi ya chini kabisa. Pili unajijengea kujiamini kwa kuwa unafanya, tofauti na pale unapokaa na kupanga pekee. Unapofanya kitu na kikakamilika, hata kama ni kidogo, unajijengea kujiamini, na baadaye utaweza kufanya zaidi kwa uzoefu ambao unakuwa umejijengea kwa kufanya.

Nikuage kwa kukuambia ya kwamba ni ruksa kabisa kuwa na ndoto na mipango mikubwa kabisa ya kibiashara au chochote unachotaka kufanya. Lakini anza kidogo, anzia chini kabisa na endelea kupiga hatua. Pale unapopata wasiwasi kwamba unaweza kushindwa, chagua kuanza na kidogo ambacho hata ukishindwa maisha yako hayatakuwa hatarini.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.