UKURASA WA 966; Kitu Pekee Unachomiliki Kwenye Maisha Yako, Unachopaswa Kukitunza Sana…

By | August 23, 2017

Kuna vitu vingi ambavyo unafikiri unamiliki kwenye maisha yako, kuanzia mali za kawaida, cheo ulichonacho, biashara uliyonayo, ajira uliyonayo na hata watu wanaokuunguka.

Lakini ukweli ni kwamba, vingi unavyofikiria kwamba unavimiliki kwa kiasi kubwa, huna umiliki navyo. Mali zinapotea, ajira zinafikia ukomo, biashara zinakufa na hata watu wanakufa.

Vitu vingi unavyong’ang’ana navyo sasa, hutaendelea kuwa navyo wakati wote wa maisha yako. Unaweza kuamka kesho na kukuta kuna mabadiliko makubwa sana ambayo yametokea kwenye maisha yako, na kuathiri yale uliyokuwa unategemea kwa kiasi kikubwa.

Lakini kipo kitu kimoja ambacho unakimiliki kwa asilimia kubwa, na unaishi nacho mpaka siku yako ya kufa. Kitu hichi ni akili yako. Akili yako iwe nzuri au mbaya, utaenda nayo maisha yako yote. Vingine vyote vitakuja na kuondoka, ila akili yako utadumu nayo wakati wote.

SOMA;

Hivyo ni muhimu sana kulinda akili yako, kwa sababu hii ndiyo utadumu nayo na itakuwezesha kupiga hatua kubwa zaidi kwenye maisha yako.

Ni muhimu mno uwekezaji wako mkubwa kuwa kwenye akili yako, kwa sababu akili hiyo ndiyo itakuletea chochote unachotaka kwenye maisha yako. Hata kama ulivyonavyo vitapotea, akili yako ikiwa sawa, itakuwezesha kuvipata tena, tena vikiwa bora zaidi.

Pamoja na umuhimu huu wa akili zetu kwenye maisha yetu, utashangaa sana kuona namna ambavyo watu hawazijali na kuzilinda akili zao.

Mtu anaweza kwenda tu kwa mazoea, asijifunze wala kuongeza maarifa yake, hapa anakosa nafasi ya kuwa bora zaidi.

Wengi zaidi wanaruhusu kila aina ya mtu kuchafua akili zao. mwenye habari hasi anawapa, mwenye habari za hofu anakaribishwa, taarifa za uongo na udaku nazo zinapata nafasi. Hii inapelekea akili kuwa hovyo, kwa sababu inapokea vitu vya hovyo.

Kama kipo kitu cha kwanza kukitunza na kukithamini sana kwenye maisha yako basi ni akili yako. Hii itakuwa na wewe kwa maisha yako yote, na itakuwezesha kupata chochote unachotaka kwenye maisha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

2 thoughts on “UKURASA WA 966; Kitu Pekee Unachomiliki Kwenye Maisha Yako, Unachopaswa Kukitunza Sana…

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.