UKURASA WA 979; Kubali, Kisha Chukua Hatua.

By | September 5, 2017

Watu wengi wanateseka katika maisha kwa sababu moja kubwa, kuna vitu hawataki kuvikubali.

Huenda ni hali walizonazo, au pale ambao wamejikuta katika kipindi fulani cha maisha yao.

Wengi hukazana kukataa, kuona kwamba wao hawastahili kupata kile ambacho wamepata.

Wengine hutafuta nani wa kumtupia lawama, nani wa kumlalamikia katika hali za aina hiyo.

Lakini haya yote yanamzuia mtu kuchukua hatua na kufanya maisha yake kuwa bora zaidi.

Hivyo anaendelea kuwa pale pale miaka nenda miaka rudi.

IMG-20170526-WA0001

Mbinu ni moja rafiki, chochote ambacho maisha yanakupa, iwe kizuri au kibaya, iwe unakipenda au hukipendi, kwanza kubali, pili chukua hatua.

Kubali pale ulipo, kwa sababu iwe umejifikisha pale wewe mwenyewe au wengine wamechangia wewe kufika pale, huwezi kukwepa kwamba uko pale.

Ni sawa na wakati ambapo unaumwa uko hoi, unachokazana siyo kujua nani kazembea ukafika pale, kwanza inabidi upone, halafu hayo mengine yatafuata ukishapona.

Kadhalika kwenye maisha yako, hasa pale mambo yanayotokea ni tofauti na ulivyotegemea.

Usijaribu kukataa, usifikiri kuna namna yaliyotokea yatabadilika na kuwa hayajatokea, badala yake kubali pale ulipo, kisha chukua hatua.

SOMA; UKURASA WA 621; Furahia Vikwazo Unavyokutana Navyo…

Ninaposema ukubali simaanishi ukubali kwamba ndiyo utaendelea kubaki pale maisha yako yote. Ninachomaanisha ni ukubali uko ambapo hukutaka kuwepo na hivyo uchukue hatua ya kutoka hapo ulipo ili kufika kule unakotaka kufika.

Dunia itakupitisha kwenye mambo magumu na usiyoyapenda, wakati mwingine utaona siyo haki kabisa wewe kupitia hayo unapitia. Lakini kama hutakubali na kuchukua hatua, utaendelea kuwa hapo ulipo. Na kadiri unavyokazana kukataa, ndivyo unavyozidi kujichimbia pale ulipo.

Kubali pale ulipo, halafu chukua hatua, hii ni njia pekee ya kuondoka popote ambapo umekwama.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.