UKURASA WA 990; Raha Na Furaha Ipo Kwenye Mchakato Na Siyo Matokeo…

By | September 16, 2017

Moja ya kazi kubwa ambazo nimekuwa najitahidi kufanya ni kupindua kila uongo ambao jamii imetujaza na kutufanya tuamini kuhusu maisha. Na kwa kujua na kupindua uongo huo, tunaujua ukweli na ukweli unatuwezesha kuwa na maisha bora na yenye mafanikio.

Leo nataka tuangalie uongo ambao kila mtu alishapandikizwa na tunaendelea kupandikizwa kila siku na kila jambo. Uongo huo ni kwamba raha na furaha zipo kwenye matokeo. Watu wanafanya kitu wakiamini kwamba wakishamaliza au kufika mwisho, basi ndiyo watakuwa na furaha mno.

Eneo

Ilianzie kwenye shule, tulienda shule tukiamini kwamba siku tunahitimu tutakuwa na furaha sana. Kweli unahitimu, na furaha unakuwa nayo kwa muda mfupi pale unapomaliza. Lakini hebu niambie, baada ya kuhitimu, ni vitu gani vinakuja kwenye kumbukumbu zako kuhusu maisha ya elimu? Kumaliza hakutakuja mara nyingi, bali yale maisha ya elimu ndiyo utakuwa unayakumbuka, na kuyakosa pia.

Utakapokutana na wenzako mliosoma pamoja, hamtahadithiana kuhusu kumaliza, bali mtahadithiana kuhusu maisha ya elimu yalivyokuwa. Mnaweza kuhadithiana na kukumbushana jambo ambalo kipindi hicho lilikuwa gumu na la kukatisha tamaa, ila sasa ukiliangalia unaona lilikuwa muhimu.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Hakuna Kisichokuwa Na Mwisho Na Mambo Muhimu Ya Kujifunza Na Kuzingatia.

Hivyo pia kwenye kazi, wengi wanafanya kazi wakiamini siku watakapostaafu basi watakuwa na furaha kubwa sana ya maisha yao. Lakini wanapostaafu kumbukumbu zao zote zinarudi kwenye kazi zao.

Ninachotaka kukuonesha hapa rafiki ni kwamba raha na furaha zipo kwenye mchakato mzima, zipo kwenye mapambano ambayo unayapitia kila siku. Achana na dunia ambayo inakutaka usahau leo na usubiri siku ya matokeo ndiyo ufurahie. Ni kweli kuna raha ya matokeo, lakini hii ni ya muda mfupi.

Fanya kila jambo kwa kuweka kila ulichonacho pale, fanya kile unachopenda na kufurahia na kila hatua unayopitia, ifurahie, ichukulie kama sehemu ya maisha yako. Usiishi maisha ya leo kama vile ni ya kupita ili ufike kwenye hatua nyingine. Bali ishi kila hatua, kwa sababu kila hatua ndiyo maisha yenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.