UKURASA WA 1016; Fursa Yako Haipo Kwenye Kazi Au Biashara Fulani, Bali Ipo Hapa…

By | October 12, 2017

Neno fursa limewapoteza watu wengi kuliko ambao limewasaidia. Hii ni kwa sababu watu wamekuwa wanakimbizana na vitu vingi wakifikiri ndiyo fursa zao. Kabla hawajapata kile walichokuwa wanakimbiza, inajitokeza nyingine ambayo inaonekana kuwa fursa nzuri zaidi. Wanaacha walichokuwa wanafanya na kuanza kukimbiza fursa hiyo mpya.

Nimekuwa nakueleza sana kuhusu hizi fursa za kukimbizana mpya kila wakati na leo nataka nikupe ukweli mwingine kuhusu fursa, ambao utakusaidia utulie na kuweza kupata kile unachotaka.

Ukweli ni kwamba, fursa haipo kwenye kazi fulani au aina fulani ya biashara, ambayo ukishaingia tu basi umefanikiwa. Kila aina ya kazi ambayo unaifahamu, kuna watu waliofanikiwa kupitia kazi hiyo na  wapo ambao wameshindwa kabisa. Kwenye kila kazi kuna watu wanaifurahia sana na wapo ambao inawapa msongo wa mawazo, hawaipendi kabisa, ila wapo tu.

Ukienda kwenye biashara hali ni hiyo hiyo, kwenye kila aina ya biashara, wapo watu waliofanikiwa sana, ambao ukiwaangalia utasema ama kweli biashara hii inalipa. Lakini pia wapo ambao wameshindwa kabisa, tena wengi mno. Wapo watu wana hamasa kubwa kwenye biashara wanayofanya, wakati biashara hiyo hiyo wapo watu wanaifanya lakini hawaipendi kabisa.

SOMA; SIKU YA 22; Akili Yako Ya Ndani Inaweza Kukufikisha Kwenye Mafanikio Makubwa.

Hivyo fursa haipo kwenye kile tunachoona ni fursa, bali fursa ipo ndani ya yule anayekwenda kufanya kile kitu.

Fursa haipo kwenye kazi wala biashara fulani, bali fursa ipo ndani yako wewe mwenyewe. Wewe mwenyewe ndiye ambaye umeibeba fursa ya mafanikio yako, ambayo ukienda popote, ukawa tayari kuweka juhudi kubwa, ukaweka muda, ukajifunza kwa kina, utaweza kupanda mpaka kufikia kileleni.

Kwenye jambo lolote, njia ya kuelekea kileleni ipo wazi, ila ni wachache wanaoichukua njia hiyo. Wengi hufikiri ukichagua kazi au biashara fulani hutasumbuka sana, mafanikio ni nje nje, na huo ni uongo mkubwa.

Mafanikio siyo kitu cha bahati kwamba labda ukiingia sehemu fulani utafanikiwa, mafanikio ni kitu cha kuchagua, ambapo unajua kipi unataka hasa, unachagua kukifanya, kwa kuweka juhudi, uvumilivu na ubunifu wa hali ya juu na unakipata. Wakati wengine wote wanakimbia, wewe unaendelea kupambana na lazima utapata unachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 1016; Fursa Yako Haipo Kwenye Kazi Au Biashara Fulani, Bali Ipo Hapa…

  1. Pingback: UKURASA WA 1025; Chagua Eneo Moja Au Machache Na Zama Ndani…. – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.