BIASHARA LEO; Biashara Inaanza Kushindwa Ndani Na Siyo Nje…

By | October 13, 2017

Katika wakati wowote ule, huwa kuna mabadiliko yanayoendelea kwenye uchumi wa nchi na hata dunia kwa ujumla. Kuna wakati uchumi unakuwa vizuri na kuna wakati uchumi unakuwa vibaya. Kuna wakati watu wana uwezo mzuri wa kununua na kuna wakati ambapo watu hawana uwezo wa kununua.

Haya ni mambo ambayo yamekuwa yanatokea tangu enzi na enzi.

Lakini katika nyakati zote, nyakati nzuri na mbaya, kuna biashara zinakua na kuna biashara zinakufa. Kuna biashara zinaanzishwa na kwenda vizuri na zipo ambazo zinaanzishwa na kufa.

Watu wengi hupata kisingizio kwamba biashara zinakufa kwa sababu ya hali mbaya ya uchumi au yale yanayoendelea.

Huo siyo ukweli, hali mbaya ya uchumi ni kitu kinachosaidia biashara kufa, lakini kifo cha biashara kinakuwa kilishaanza ndani ya biashara yenyewe.

Ukweli ni kwamba, hata uchumi uwe mgumu kiasi gani, biashara zote haziwezi kufa, kuna biashara ambazo zitapona na hata kuwa imara zaidi. Na wakati mwingine kuna biashara zinakua zaidi kwenye nyakati ngumu kiuchumi.

Hii ndiyo sababu ni muhimu sana kuendesha biashara zetu katika misingi imara, misingi ambayo itaiwezesha biashara kuwa imara kila wakati.

Kwa mfano hali inapokuwa ngumu, biashara zinazoanza kuathirika kwa kasi ni zile ambazo haziendeshwi kwa misingi. Zile ambazo hazina tatizo kubwa la watu zinatatua, haziendeshwi kwa uaminifu na hakuna mpango wa udhibiti wa mzunguko wa fedha, zinaumia sana.

Tengeneza usimamizi mzuri wa biashara yako wakati wowote ule, dhibiti sana mzunguko wa fedha na matumizi, hakikisha matumizi yanakuwa madogo na ya muhimu pekee, wakati wowote ule na siyo wakati mgumu pekee.

Yaani vitu hivi vinapaswa kuwa ni sehemu ya biashara, tabia ambayo imeshazoeleka.

Mwekezaji na bilionea Warren Biffet anasema ukisikia mfanyabiashara anasema sasa naanza kudhibiti matumizi, jua ameshachelewa. Hicho kinapaswa kuwa kitu ambacho anafanya kila siku kwenye biashara yake.

SOMA; BIASHARA LEO; Msimu Wa Biashara Yako.

Ijue misingi ambayo biashara yako inasimamia kila wakati, kuanzia kile ambacho biashara inafanya, utoaji wa huduma kwa wateja, udhibiti wa mzunguko wa fedha na wasaidizi wanaojituma na waaminifu.

Haya yatasaidia biashara kwenda vizuri hata kama hali ya uchumi ni ngumu, wakati huo zile biashara zinazoendeshwa kwa mazoea bila ya msingi zikiwa zinakufa.

Warren Buffet pia amewahi kusema ni pale mawimbi yanapotulia ndiyo unaweza kuona nani anaogelea uchi. Akiwa na maana kwamba wakati mambo yanaenda vizuri, kila mtu ataonekana yuko vizuri, anafanya vizuri. Lakini mambo yanapokuwa mabaya, ndipo sasa wale ambao hawapo vizuri wanaonekana wazi. Hivyo hali mbaya ya uchumi ni kitu kinachotusaidia kuona biashara zipi zinaendeshwa vizuri na zipi haziendeshwi vizuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: BIASHARA LEO

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.