UKURASA WA 1022; Acha Kujiua Kwa Kiu Huku Umezungukwa Na Maji Safi Na Salama…

By | October 18, 2017

Umeshawahi kusikia mtu anakufa kwa kiu huku akiwa amezungukwa na ziwa lenye maji masafi kabisa ya kunywa?

Unaweza kushangaa na kusema mtu anawezaje kukubali afe kwa kiu wakati maji yamemzunguka. Lakini hii ndiyo hali ambayo tunaiishi kwenye dunia ya sasa.

Tunaishi kwenye zama za taarifa, zama ambazo kuna taarifa nyingi zinazalishwa ndani ya siku moja, kuliko taarifa zilizokuwa zinazalishwa mwaka mzima kipindi cha miaka 100 iliyopita.

Lakini pamoja na upatikanaji huu kwa wingi wa taarifa, bado watu wengi hawana maarifa sahihi ya kuweza kuyafanya maisha yao kuwa bora.

Watu wanaendelea kuwa na maisha magumu, maisha ya mateso na wasiyoyapenda, wakiwa hawana hatua ya kuchukua, wakati wamezungukwa na kila fursa ambayo inawawezesha kujifunza hatua za kuchukua.

Hii ndiyo sababu tunasema watu wanakufa kwa kiu wakiwa wamezungukwa na maji. Taarifa zipo nyingi, ambazo mtu angejifunza na kufanyia kazi, maisha yake yangekuwa bora sana.

Matatizo makubwa kabisa ni mawili;

Tatizo la kwanza ni kutokuyapata maarifa na taarifa zilizopo. Hapa mtu hajisumbui kujifunza wala kutafuta taarifa na maarifa sahihi kwa kile anachotaka kwenye maisha yake. Anafanya kile ambacho amezoea kufanya, licha ya kuwepo kwa njia za kufanya kwa ubora zaidi. Hili ni tatizo ambalo linachochewa na uvivu na kutokujua pia.

Tatizo la pili ni kuyapata maarifa lakini kutokuchukua hatua kulingana na maarifa hayo. Hapa mtu anajifunza lakini hachukui hatua. Anajua kila kitu anachopaswa kufanya ili kupata matokeo anayotaka kupata, lakini hachukui hatua. Hapa ni sawa na mtu mwenye kiu, ambaye amezungukwa na maji, anayanywa maji, halafu anayatema. Haileti msaada wowote kwenye kiu yake.

SOMA; Kozi 1100 Unazoweza Kujifunza Bure Kupitia Mtandao.

Chukua muda wako kujifunza, jifunze kila siku, dadisi, hoji na kuwa mbunifu. Kwa chochote unachofanya, angalia njia ya kuwa bora zaidi.

Chochote unachojifunza, kifanyie kazi, na kifanyie kazi mara moja, usisubiri, kwa sababu kitapotea. Kifanyie kazi kwa kukijaribu kwako mwenyewe, kubadili namna unavyofikiri na hata kuwafundisha wengine.

Kama unajifunza kitu halafu hukifanyii kazi, ni bora usijifunze kabisa, kwa sababu hakitakuwa na msaada wowote kwako. Utakuwa umeamua tu kupoteza muda wako. Naweza kusema usijisumbue kujifunza kitu ambacho hutakifanyia kazi, usijisumbue kabisa, haitakuwa na msaada wowote kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.