3015; Simba na kondoo.

3015; Simba na kondoo.

Rafiki yangu mpendwa,
Mtu mmoja amewahi kusema unapaswa kuhofia zaidi kundi la kondoo 100 wanaoongozwa na simba mmoja kuliko unavyohofia kundi la simba 100 wanaoongozwa na kondoo mmoja.

Hiyo ni kauli iliyobeba ujumbe mzito sana inapokuja kwenye uongozi na timu kwenye biashara.
Ubora na ufanisi wa timu inayoendesha biashara unategemea sana uimara wa kiongozi wa biashara hiyo.

Jinsi timu ya biashara ilivyo ni kivuli cha kiongozi wa timu hiyo.
Kama kiongozi wa biashara ni jasiri na imara, hivyo pia ndivyo timu nzima inavyokuwa.
Lakini kama kiongozi ni mwoga na dhaifu, timu nayo itakuwa hivyo hivyo.

Haijalishi unaanza na timu ya aina gani, baada ya muda timu hiyo itaakisi vile ulivyo wewe.
Hiyo ni kwa sababu watu hawafanyi yale unayowaambia wafanye, bali wanafanya yale wanayoona wewe unafanya.

Unaweza kupiga kelele sana wafanye nini.
Unaweza kutoa miongozo mbalimbali ambayo wanapaswa kufuata.
Lakini mwisho wa siku, watu watafanya kile unachofanya na siyo tofauti na hapo.

Ndiyo maana hata biashara na taasisi kubwa ambazo tayari zina miongozo ya jinsi kila kitu kinavyopaswa kufanya, bado matokeo yanayozalishwa yanategemea sana uongozi unaokuwepo. Na ndiyo maana mara kwa mara viongozi wa taasisi hizo hubadilishwa ili kubadili matokeo.
Ingekuwa miongozo pekee inatosha, kusingekuwa na umuhimu wa kuwepo kwa kiongozi.
Lakini licha ya uwepo wa miongozo hiyo, bado uongozi ni muhimu sana, maana ndiyo unaowasukuma watu kufanya kwa ubora zaidi.

Kadhalika hata nchi zenye katiba nzuri, ambazo zinawapa miongozo sahihi kwa viongozi kuifuata na hata kuwabana wasitoke nje ya miongozo hiyo, bado hatua ambazo nchi itapiga zinategemea sana kiongozi anayekuwepo.

Haya yote yanapaswa yakutafakarishe sana wewe na biashara uako.
Aina ya watu ulionao na jinsi wanavyofanya, inaakisi wewe ni kiongozi wa aina gani.
Haijalishi unaanza na watu imara au dhaifu kiasi gani, wale unaoenda nao, wanakupa kile ambacho wewe ndiyo unacho.

Tukianza na namna unavyowapata watu wako, inategemea sana na wewe ni mtu wa aina gani.
Mara zote unapata watu unaowakubali au unaowavumilia.
Hiyo ina maana kama viwango vyako ni vya chini sana, utapata watu wa viwango hivyo. Na kama viwango vyako ni vya juu, utapata wa aina hiyo pia.

Baada ya kuwapata watu, kadiri unavyokwenda nao, watabadilika na kuwa kama wewe zaidi kuliko kubaki vile walivyokuwa.
Na bila hata ya wewe kujua, utajikuta unawapenda wanaokuwa kama wewe na kutowapenda wasiokuwa kama wewe.
Hilo linafanya wengi wakazane kuwa kama wewe na wale wasioweza basi kuondoka kama wewe hutawaondoa.

Mwisho wa siku unajikuta umebaki na timu ambayo ipo kama wewe kwenye maeneo mengi na hivyo matokeo unayopata yanatokana na timu hiyo ambayo imetokana na wewe.

Kama unataka kubadili kitu chochote kwenye biashara, anza kwa kubadilika kwanza wewe kiongozi wa biashara.
Anza kwa kujiwekea wewe mwenyewe viwango vipya na kujisukuma kuvifikia.
Ghafla utashangaa timu nayo inapambana kufikia viwango hivyo vipya na wale wasioweza wakikimbia wenyewe.

Wewe binafsi unaiathiri timu yako kwa viwango vikubwa sana.
Hivyo matokeo yoyote ambayo timu yako inakupa, usiilaumu timu, bali angalia ni jinsi gani wewe kama kiongozi umeathiri timu hiyo na matokeo hayo.

Chagua kuwa simba mmoja unayeongoza kundi la simba wengine 100, baada ya kuanza nao wakiwa kama kondoo.
Badala ya kuwa kondoo mmoja unayeongoza simba 100, maana yatakuwa matumizi mabaya ya rasilimali ambazo utaishia kuziharibu.

Wito wangu mkubwa kwa kila mmoja wetu ni tuache kuziharibu timu zetu.
Tunazembea sana kwenye hili eneo na kujikuta tumeharibu sana timu nzuri tulizoanza nazo.
Tuzingatie haya ili tuweze kujenga timu imara.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe