Barua ya XVI; Falsafa kama mwongozo wa maisha.

By | August 18, 2023

Barua ya XVI; Falsafa kama mwongozo wa maisha.

Rafiki yangu Mstoa,
Watu wengi wanaposikia kuhusu falsafa, huwa wanafikiria watu wenye akili na uelewa mkubwa wa mambo ambao wanabishana maswali magumu ya maisha kama nini maana ya maisha, nini kinatokea baada ya kifo n.k.

Kwa baadhi ya falsafa ndivyo mambo yalivyo. Lakini inapokuja kwenye falsafa ya Ustoa, mambo ni tofauti kabisa.
Falsafa ya Ustoa siyo ya kubishana kuhusu maswali magumu ya maisha.
Bali ni falsafa ya kutuongoza namna bora ya kuendesha maisha yetu.

Ustoa ni falsafa ya vitendo, ambayo inatupa hatua za kuyaishi maisha yetu kwa namna bora ili yawe ya mafanikio na tuweze kuyafurahia.

Katika kufafanua hilo la matumizi ya falsafa kama mwongozo wa maisha, mwanafalsafa Seneca aliandika barua kwa rafiki yake Lucilius.
Kupitia barua hiyo tunakwenda kujifunza hatua za kuchukua ili falsafa ya Ustoa iweze kuwa mwongozo sahihi wa maisha yetu.

1. Huwezi kuwa na maisha ya furaha bila falsafa.

Seneca anaianza barua kwa kumhakikishia rafiki yake Lucilius kwamba hakuna mtu anayeweza kuwa na maisha ya furaha kama hana hekima. Na chanzo cha hekima ni falsafa.
Na ili mtu ajifunze falsafa, lazima atenge muda wa kusoma na kutafakari yale anayojifunza kwa namna anavyokwenda kuyatumia kwenye maisha yake.
Hekima ni maarifa kwenye vitendo, hivyo kujifunza tu haitoshi, lazima mtu uchukue hatua ndiyo uweze kunufaika na yale uliyojifunza.
Na hivyo ndivyo mtu anavyoitumia falsafa kama mwongozo wa kujenga maisha bora kwake.

Hatua ya kuchukua;
Tenga muda wa kujifunza falsafa ya Ustoa na kutafakari yale uliyojifunza na hatua unazokwenda kuchukua.
Kila siku chukua hatua za Kistoa kwenye maisha yako ili yawe bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.

Nukuu;
“It is clear to you, I am sure, Lucilius, that no man can live a happy life, or even a supportable life, without the study of wisdom.” – Seneca

“Ni dhahiri kwako Lucilius, kwamba hakuna mtu anayeweza kuishi maisha ya furaha bila ya kujifunza hekima.” – Seneca

2. Falsafa siyo kwa ajili ya kujionyesha.

Seneca anamtaka Seneca aitumie falsafa kujiendeleza binafsi badala ya kuitumia kujionyesha kwamba anajua vitu vingi.
Anamwambia wazi kwamba hatua ambazo mtu anapiga huwa zinaonekana dhahiri, hazihitaji hata mtu ajieleze sana.
Anaendelea kusisitiza lengo la falsafa ni kujitathmini, kujihoji na kujifuatilia kwa umakini kwenye kila ambacho mtu unafanya ili kuona kama kweli unaishi kwa misingi uliyochagua kuishi nayo.
Falsafa inatuongoza nini tunapaswa kufanya na nini hatupaswi kufanya.
Kwa kuizingatia misingi hiyo ya kifalsafa, tunaweza kujenga maisha bora kabisa.
Ili kujua kama tunazingatia misingi hiyo, lazima tujifanyie tathmini na kujihoji kwa kila tunachofanya.

Seneca anasema kuna mambo mengi yanayotokea kwenye maisha ambayo tungependa kupata ushauri wa namna bora ya kuyakabili. Ushauri mzuri unapatikana kwenye falsafa.
Hiyo ina maana kama tukiishi vizuri misingi ya falsafa, kwenye kila hali tutajua kipi sahihi kufanya. Kamwe hatutakwama.

Hatua ya kuchukua;
Usihangaike kutumia maneno kueleza jinsi unavyoiishi falsafa ya Ustoa. Badala yake iishi falsafa hiyo kwa vitendo na matokeo yatajidhihirisha yenyewe. Kama kweli unaiishi misingi ya falsafa, hatua unazopiga zitaonekana dhahiri.

Nukuu;
“Countless things that happen every hour call for advice; and such advice is to be sought in philosophy.” – Seneca

“Mambo mengi yanayotokea kwenye kila saa ya maisha yanataka ushauri wa kuyakabili; na ushauri huo unapatikana kwenye falsafa.” – Seneca

3. Falsafa ina umuhimu kama hatima ya maisha ya mtu imeshapangwa?

Watu wamekuwa wanaamini kwamba hatima ya maisha yao tayari imeshapangwa kabla hata hawajazaliwa.
Watu wa dini wanaamini Mungu alishapanga maisha ya mtu yatakuwaje hapa duniani tangu kuzaliwa mpaka kufa.
Watu wasio wa dini wanaamini asili imeshapanga hatima ya maisha ya mtu hapa duniani.
Kwa sababu hiyo, wengi huona hawahitaji kujisumbua na falsafa kwa sababu hawawezi kubadili hatima yao ambayo tayari imeshapangwa.

Seneca anatuambia haijalishi kama hilo la hatima ni kweli au si kweli, wajibu wetu ni kuishi kwa falsafa.
Iwe tuna hatima iliyopangwa au hatuna, kuishi kwa misingi ya falsafa kunayaboresha maisha tuliyonayo na hilo ndiyo muhimu zaidi.
Wajibu wetu ni kufanya yale yaliyo ndani ya uwezo wetu na kuacha kujihangaisha na yale yaliyo nje ya uwezo wetu.
Hatupaswi kujisumbua kuhusu hatima yetu, hicho ni kitu ambacho kipo nje ya uwezo wetu.
Tunapaswa kujisumbua na misingi tunayoiishi kwenye kila siku ya maisha yetu, hiyo ipo ndani ya uwezo wetu kabisa.
Na kuchagua kuiishi misingi ya kifalsafa hasa ya Ustoa, kunayafanya maisha yetu kuwa bora.

Hatua ya kuchukua;
Acha kusumbuka na mambo yaliyo nje ya uwezo wako kama kuhusu hatima ya maisha yako.
Hangaika na kudhibiti yaliyo ndani ya uwezo wako kama kuishi kwa misingi ya falsafa ya Ustoa.
Kilicho muhimu kwako kwa sasa ni kuwa na maisha bora, ambayo utaweza kuyajenga kupitia kuishi misingi ya falsafa.

Nukuu;
“Whether the truth, Lucilius, lies in one or in all of these views, we must be philosophers; whether Fate binds us down by an inexorable law, or whether God as arbiter of the universe has arranged everything, or whether Chance drives and tosses human affairs without method, philosophy ought to be our defence.” Seneca

“Iwe kuna ukweli au la kwamba hatima ya maisha yetu imepangwa na Mungu au asili, tunapaswa kuwa wanafalsafa. Falsafa inapaswa kuwa njia yetu ya kujilinda na hayo yote.” – Seneca

4. Ukiishi kwa asili kamwe hutakuwa masikini, ila ukiishi kwa tamaa kamwe hutakuwa tajiri.

Seneca anamnukuu mwanafalsafa Epicurus ambaye alikuwa wa falsafa pinzani na ya Ustoa, ila aliamini kitu sahihi ni sahihi hata kama kimesemwa na mtu asiye sahihi.
Epicurus alisema mtu anayeishi kwa misingi ya asili kamwe hawezi kuwa masikini. Wakati yule anayeishi kwa maoni na tamaa zake mwenyewe kamwe hawezi kuwa tajiri.

Seneca anafafanua hilo kwa kusema mahitaji ya asili ni machache na yanayojitosheleza. Mtu akizingatia hayo anakuwa na utoshelevu kwenye maisha yake.
Lakini mahitaji ya tamaa huwa ni mengi na hayana ukomo, kwani kadiri mtu anavyopata, ndivyo anavyotamani kupata zaidi na zaidi. Hivyo mara zote atajiona bado ni masikini kwa sababu hajapata alichotaka.

Seneca anaendelea kufafanua akisema ikitokea mtu umepewa mali zote za mtu tajiri na ukaweza kuwa na kila unachotaka, hilo litaibua tamaa ya kutaka kupata zaidi na zaidi.
Hivyo haitakupa kuridhika, bali itakupa tamaa zaidi. Na tamaa ndiyo zinamfanya mtu ajione ni masikini mara zote.

Hatua ya kuchukua;
Ishi kwa kutimiza mahitaji yako ya msingi ambayo ni machache na yanajitosheleza. Juhudi unazokuwa unaweka ili kufanikiwa zaidi zisiwe kwa ajili ya tamaa binafsi, bali kwa ajili ya kuwa na mchango kwa wengine.
Ukiweza kuondokana na tamaa, tayari unakuwa umefanikiwa, bila kujali umepata nini.

Nukuu;
“If you live according to nature, you will never be poor; if you live according to opinion, you will never be rich.” – Epicurus

“Kama utaishi kulingana na asili, kamwe hutakuwa masikini; ila kama utaishi kulingana na tamaa, kamwe hutakuwa tajiri.” – Epicurus

5. Mara zote hakikisha upo kwenye njia sahihi.

Tukiyachukulia maisha kama safari, huwa tunayaanza tukijua wapi tunakotaka kufika. Kisha tunaingia kwenye njia ya kutufikisha kule tunachotaka.
Lakini cha kushangaza, muda unakwenda na hatufiki kwenye safari yetu.
Kwa bahati mbaya sana hatusimami na kujiuliza kama tupo kwenye njia sahihi au la. Na hilo linapelekea tuzidi kupotea.

Seneca anatuambia kwamba pale tunapokuwa kwenye safari ambayo tumekwenda kwa muda mrefu ila hatuuoni mwisho, basi tujue tumeshapotea.
Tujue tumetoka kwenye njia yetu kuu ambayo ni kuishi kulingana na asili na kwenda njia ya upotevu ambayo ni kuendeshwa kwa tamaa.
Kama ambavyo tumeshaona, tamaa hazina mwisho. Hivyo kadiri mtu anavyozidi kuzikimbiza tamaa, ndivyo anavyozidi kupotea kwenye njia yake kuu.

Njia kuu ni kuishi kulingana na asili. Ambayo ina mahitaji machache ya msingi na yanayotimilika.
Njia ya upotevu ni kuishi kulingana na tamaa. Ambapo mahitaji ya tamaa huwa yanaendelea kukua kadiri mtu unavyoyatimiza.

Hatua ya kuchukua;
Mara kwa mara jikague kwenye safari yako ya maisha kuona kama upo kwenye njia sahihi au la. Unakuwa kwenye njia sahihi, ambayo ni kuishi kwa asili, pale unapouona mwisho wa safari.
Na unakuwa kwenye njia ya upotevu, ambayo ni kuishi kwa tamaa, pale unapokuwa huuoni mwisho wa safari.
Unapogundua haupo kwenye njia sahihi, simama na urudi kwenye njia sahihi ili uweze kuwa na maisha bora na unayoyafurahia.
Na hiyo haimaanishi usipambanie makubwa, bali inamaanisha usiyapambanie kwa tamaa.

Nukuu;
“If you find, after having travelled far, that there is a more distant goal always in view, you may be sure that this condition is contrary to nature.” – Seneca

“Kama baada ya kusafiri kwa umbali mrefu unajikuta kwamba kuna malengo ya mbali zaidi, unaweza kuwa na uhakika kwamba hali hiyo ni kinyume na asili.” – Seneca.

Rafiki yangu Mstoa, tumechagua njia sahihi kabisa kuiishi falsafa hii ya Ustoa.
Tuiweke falsafa hii kwenye matendo ili tuweze kujenga maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa.
Tuishi kulingana na asili na siyo kuendeshwa na tamaa.
Kwa kuzingatia msingi huo muhimu wa falsafa, tutaendelea kuyafurahia maisha huku tukipiga hatua kubwa zaidi.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.

Category: FALSAFA YA USTOA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

16 thoughts on “Barua ya XVI; Falsafa kama mwongozo wa maisha.

  1. Alex Kamata#MchinaWaMwanza

    Ukiishi kwa asili kamwe hutakuwa masikini, ila ukiishi kwa tamaa kamwe hutakuwa tajiri.

  2. dickson paulo

    Maisha yanataka uyaishi kama asili inavyotaka na siyo watu wanavyotaka na kama mungu kapanga tunatakiwa tupambane tueeze kuwashangaza wale aanaosema haiwezekaji

  3. nderahisho

    Ukiishi kwa asili kamwe huwezi kuwa maskini, na ukiishi kwa tamaa kamwe huwezi kuwa tajiri.

    Epicurus.

  4. ernest74

    Hakika ustoa ndio falsafa Bora kabisa kwenye zama hizi tuishi kulingana na asili na Wala Sio tamaa
    Asante

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.