UKURASA WA 722; Huwezi Kuziba Pengo Na Vitu…

By | December 22, 2016

Umewahi kusikia watu wakilalamika kwamba fedha hazileti furaha? Na wengine wakisema kwamba matajiri wana kila kitu isipokuwa amani ya moyo?

Umewahi kusikia pia watu wakilalamika kwamba kuoa au kuolewa kumewaondolea furaha na uhuru kwenye maisha yao.

Umewahi kusikia pia, au kukutokea wewe mwenyewe, kujikuta unakimbiza kitu kimoja, baada ya kukipata ukajiona kama safari ndiyo inaanza? Yaani mwanzo mafanikio kidogo yalikuwa yanakuridhisha, lakini kadiri unavyofanikiwa ndiyo unajiona kama bado kabisa?

SOMA; Pengo Ulilonalo Sasa…

Hizi zote ni hali zinazotokana na kulazimisha mambo ambayo hayawezekani. Na jambo kubwa tunalolazimisha ni kutaka kuziba pengo kwa vitu, kitu ambacho hakiwezekani.

Kila mmoja wetu ana pengo ndani yake, kuna hitaji fulani lipo ndani yetu, ambalo kama hitaji hili halitatimizwa, basi maisha yetu yote yatakosa maana. Hata kama tutapewa kila tunachokitaka, kama hitaji la mioyo yetu halitatimia, basi maisha yetu yatakuwa hovyo.

Makosa makubwa tunayofanya ni kufikiri pengo hili linaweza kuzibwa na vitu au watu. Na ndiyo maana watu wanatafuta fedha wakijua wakishazipata fedha basi watakuwa na furaha. Au watu wengine wanaoa au kuolewa wakiamini kwa kufanya hivyo watakuwa na maisha ya furaha.

Mtego uko hapa, pengo lililopo ndani yako, utaliziba wewe mwenyewe, na siyo vitu au watu wengine watakaokuja kwenye maisha yako.

SOMA; Mpaka Lini?

Kwa mfano, sehemu kubwa ya pengo lililopo ndani yetu ni kutaka furaha. Kila mtu anapenda furaha kwenye maisha yake. Lakini furaha ya kweli haitokani na vitu unavyomiliki au watu wanaokuzunguka. Bali furaha inaanzia ndani yako mwenyewe, kwa kujikubali na kuridhishwa na maisha yako, kwa namna yalivyo.

Kama huna furaha kabla hujafanikiwa, basi huwezi kuwa na furaha ukishafanikiwa. Kama huna furaha kabla hujaoa au kuolewa, basi jua kuoa au kuolewa hakutakuletea furaha. Furaha ni kazi ya ndani yako mwenyewe, inayotokana na namna unavyoyachukulia maisha, mtazamo ulionao na mawazo yanayotawala akili yako.

Pengo jingine kubwa tulilonalo ndani yetu ni uhuru. Kila mtu anapenda kuwa huru, kila mtu anapenda kuendesha maisha yake kwa namna ambayo inamfaa yeye. Kwa kukosa uhuru, hakuna kitu kinaweza kuyafanya maisha kuwa bora. Na uhuru pia unaanzia ndani yako mwenyewe, unaanzia kwenye mawazo yako, mtazamo wako na namna unavyoyachukulia mambo.

Vitu vya nje haviwezi kukuletea uhuru kama ndani yako haupo huru.

Tuache sasa kulazimisha mambo ambayo hayaendani. Tuache kutegemea vitu vya nje kuziba mapengo yaliyopo ndani yetu. Tuchukue juhudi za makusudi, sisi wenyewe kuhakikisha tunaziba mapengo haya. Kwa kuweka juhudi kubwa, kubadili mitazamo yetu na kujikubali kwa pale tulipo na kile tunachofanya. Kwa kuanzia hapo tunaweza kufanya makubwa zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.