UKURASA WA 757; Nenda Kinyume Na Sababu Ulizonazo, Leo Tu…

By | January 26, 2017

Hakuna mtu ambaye hana ndoto kubwa, au hata kama siyo kubwa, basi angalau kila mtu ana taswira ya maisha yake mazuri, anajiona siku zijazo akiwa pazuri kuliko alipo sasa.

Hakuna mtu ambaye hapendi mafanikio, kila mtu anapenda kuwa bora zaidi leo kuliko alivyokuwa jana.

Lakini kama ulivyo uhalisia wa maisha, kupenda na kupata kile unachopenda ni vitu viwili tofauti. Unaweza kupenda au kuwaza kile unachotaka, lakini kukipata hasa, kazi inahitajika, tena siyo kazi ya kitoto, ni kazi hasa.

Kwa kuwa kazi inachoshwa, na kwa kuwa kazi inamaanisha tunahitaji kuacha baadhi ya vitu tunavyofanya sasa ili kupata kile tunachotaka kufanya, huwa tunatafuta sababu ya kupeleka mbele kazi hiyo, angalau kwa sasa.

Tunapata sababu kwa nini hatuwezi kuanza biashara sasa, labda hali ni ngumu, au siyo wakati sahihi, au miezi fulani utakuwa vizuri zaidi.

Unapata sababu za kujiridhisha kabisa kwa nini huwezi kuanza kuweka akiba na kuwekeza sasa hivi, kwamba una matumizi makubwa, kwamba kipato n kidogo na kwamba utaanza kufanya hivyo kipato kikishaongezeka.

SOMA; Kuwa Na Maisha Bora, Nenda Kinyume na Tabia Za Asili Za Binadamu.

Unajua kabisa kufanya mazoezi ni muhimu kwa afya yako, lakini unazo sababu kwa nini hufanyi mazoezi, labda huna muda wa kutosha kwa sasa, au huna vifaa vya kufanya mazoezi.

Sababu zimekuwa hazikosekani, na sababu zimekuwa kikwazo kwa wengi kuchukua hatua.

Sasa ninachotaka ufanye leo ni kwenda kinyume na kila sababu uliyonayo, leo tu.

Yaani leo, chagua kitu ambacho utakifanya, licha ya sababu ya kutokufanya ambayo unayo. Una sababu kabisa kwa nini huwezi kufanya sasa, kubaliana na sababu hiyo, halafu anza kufanya. Anza kufanya kwa kujiahidi ni leo tu. Utashangaa kitu kikubwa sana, kwamba sababu ulizonazo imekuwa njia ya wewe kujificha tu, siyo sababu halisi kwa sababu muda wowote unaweza kuchagua kufanya kile unachotaka kufanya.

Chukua hatua leo, anza na chochote kidogo, chagua kukifanya japo una sababu ya kutokufanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.