UKURASA WA 994; Siyo Mwanzo Na Wala Siyo Mwisho…

By | September 20, 2017

Maisha yetu ni mwendelezo wa mambo ambayo hayana mwanzo wala mwisho. Maisha yetu yana mwanzo pale tunapozaliwa na yana mwisho pale tunapokufa. Lakini hapo katikati, mambo tunayokutana nayo kwenye maisha yetu, hayana mwanzo wala mwisho.

Nakushirikisha hili rafiki kwa sababu watu tumekuwa tukijidanganya kwamba kama tukiweza tu kutoka pale tulipo sasa, basi kila kitu kitaenda sawa. Kama tu tukiweza kutatua changamoto inayotukabili sasa, basi maisha yetu hayatakuwa tena na changamoto.

IMG-20170505-WA0011

Ukweli ni kwamba mambo yanatokea na mambo yataendelea kutokea, hayana mwanzo wala hayana mwisho. Unaweza kuona changamoto ulizokuwa nao zimeisha lakini haipiti muda zikaibuka changamoto nyingine. Unaweza kufikiri kesho itakuwa bora zaidi ikaendelea kuwa kama leo.

Mambo haya yanayotutokea sasa kwenye maisha, yamekuwa yanawatokea watu tangu enzi na enzi. Changamoto za maisha hapa duniani ni zile zile, tangu enzi na enzi, kinachobadilika ni mazingira na vichocheo vya changamoto hizi.

SOMA; UKURASA WA 913; Vikwazo Vya Wengine, Ni Fursa Nzuri Kwako…

Hivyo tusijidanganye kwamba ipo siku tutaamka na kukuta changamoto zetu zote zimefika mwisho, zote zimemalizika na maisha yetu ni raha mustarehe.

Kwa kujua hili, kwamba haya mambo hayana mwanzo wala mwisho, yamekuwa yanatokea na yataendelea kutokea, inatusaidia kugundua jambo moja uhimu sana. Jambo hilo ni kwamba, pale tulipo sasa ndiyo sehemu muhimu zaidi ya maisha yetu.

Siyo tulipokuwa jana, kwa sababu hakuna tunachoweza kubadili kuhusu jana. Na wala siyo tutakapokuwa kesho, kwa sababu hatuna uhakika wa hiyo kesho. Pale tulipo sasa, kwa kile ambacho tunafanya, ndiyo muhimu zaidi kwetu.

Ni vyema tukatambua hili na kutumia vizuri wakati tulionao kwenye maisha yetu. Tuache kujidanganya kwamba tunateseka sasa ili kesho mambo yawe mazuri. Tunapaswa kuyaishi maisha yetu sasa, tukiweka juhudi tunazoweza kuweka sasa, ili kuyafanya kuwa bora zaidi.

Chochote unachopitia, jua kwamba hakina mwanzo wala hakina mwisho, kimekuwa kinatokea na kitaendelea kutokea, hivyo ni vyema ukakazana kuishi leo, kuwa bora leo na kuchukua hatua za kuweza kufanya maisha kuwa bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 994; Siyo Mwanzo Na Wala Siyo Mwisho…

  1. Pingback: UKURASA WA 1095; Hatari Iliyopo Kwenye Mtazamo Wa Kusaka Fursa… – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.