UKURASA WA 1025; Chagua Eneo Moja Au Machache Na Zama Ndani….

By | October 21, 2017

Moja ya changamoto za zama tunazoishi sasa, ni wingi wa fursa, wingi wa vitu vya kufanya na wingi wa mambo yanayotuvutia, yanayotushawishi kwamba ni mazuri zaidi kwetu.

Na hili limekuwa linatuzuia kufanikiwa kwa sababu watu wamekuwa wanatumia muda mwingi kujaribu mambo mapya na yanayoonekana ni mazuri, kuliko muda wanaotumia kwenye jambo moja na kuhakikisha wanalielewa vizuri.

Wapo watu leo watakuja kwako na kukuambia kitu hichi ni fursa nzuri, kinalipa sana na unapaswa kukifanya. Haitapita muda watu hao hao watakuja na fursa nyingine ambayo ni nzuri zaidi, watakuambia sahau ile, habari hasa ni hii hapa na watakuonesha kwa nini hiyo ni bora zaidi.

Kuna fursa nyingi, nafasi nyingi, biashara nyingi na hata mambo mengi ya kufanyia kazi kuliko uwezo tulionao na muda wetu pia.

Watu wengi wanachofanya ni kuruka ruka kutoka fursa moja kwenda nyingine, wanapata wazo moja wanaanza kulifanya, wanapoanza mwanzo mambo yanakuwa mazuri, wanapoendelea kwenda wanakutana na changamoto. Badala ya kutatua changamoto ile, wanaangalia fursa ipi nyingine rahisi zaidi. Na kwa kuwa zipo nyingi, hawakosi, wanaingia kwenye fursa nyingine.

Mchezo unakua huo, miaka nenda miaka rudi mtu yupo pale pale, anajaribu kila aina ya biashara lakini hapigi hatua ya mafanikio.

SOMA; UKURASA WA 1016; Fursa Yako Haipo Kwenye Kazi Au Biashara Fulani, Bali Ipo Hapa…

Ukweli ni kwamba, hutaweza kufanikiwa kwa kujaribu kila aina ya fursa inayokuja mbele yako.

Mafanikio yanakuja kwa kuchagua eneo moja, au machache, na kuzama ndani kwelikweli, kulielewa kwa undani, kuweka juhudi kubwa, kuzama kiasi cha kuwa mbobezi wa eneo hilo na hapo ndipo unapoweza kufanya makubwa.

Hutapata maziwa mengi na mazuri kwa kukusanya ng’ombe wasiokuwa na afya, kukamua na yakiisha unakimbilia kwa ng’ombe mwingine. Bali unapata maziwa mengi na mazuri kwa kuchagua ng’ombe bora, kuwalisha vizuri na kuwapa huduma zote, halafu na wao wanakupa maziwa.

Hivi ndivyo ilivyo kwenye fursa za mafanikio, hakuna fursa ambayo haihitaji kazi, hakuna fursa ambayo haihitaji muda wako na hakuna fursa ambayo ni rahisi, unapata tu kile unachotaka na haraka.

Ni rahisi kuona fursa mpya ni rahisi kabla hujaingia, lakini ukishaingia ndipo unapoona changamoto zake.

Acha kukimbizana na kila aina ya fursa, changua moja au chache na nenda ndani zaidi, chimba zaidi. Usiogope kusema hapana kwa fursa mpya zinazokuja, hutakosa mengi. Badala yake utajiweka kwenye mazingira ya kupata makubwa zaidi baadaye kwa kutulia na fursa moja.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply