UKURASA WA 669; Toa Toa Toa… Omba.

By | October 30, 2016

Kanuni za maisha bora na ya mafanikio tunazojifunza sasa, siyo mpya, bali zimekuwepo tangu enzi na enzi. Tangu kuwepo kwa maisha ya binadamu, kanuni hizi zimekuwepo. Zimekuwa zinaleta majibu mazuri kwa wale wanaozitumia na kuleta majibu mabaya kwa wale ambao hawazizingatii.

Watu wamekuwa wakipuuza na kutozingatia kanuni ndogo na muhimu sana kwa mafanikio, na hii imekuwa inawapelekea kushindwa kuwa na yale maisha ambayo wanataka kuwa nayo.

Moja ya kanuni ambazo wengi wamekuwa hawaizingatii ni kanuni ya kutoa na kupata.

Kanuni ni kwamba unapata sawa sawa na unavyotoa, yaani utapata, lakini lazima kwanza utoe. Na siyo kinyume chake. Lakini cha kushangaza, watu wengi wamekuwa wakitumia kanuni hii kinyume, wamekuwa wakitaka kupokea kwanza ndiyo na wao watoe.

Kwamba kama wapo kwenye ajira, mshahara uongezwe kwanza ndipo wafanye kazi kwa bidii. Na kama wapo kwenye biashara basi wateja watoe kwanza fedha ndipo yeye awape huduma bora.

Hii ni kinyume na kanuni na yeyote atakayejaribu kufanya hivyo hawezi kamwe kufanikiwa, hata ikitokea amefanikiwa, mafanikio yake hayatadumu.

Kanuni ni kwamba utoe kwanza, ndipo uweze kupokea.

Sasa kuna huu upande wa pili, ambao wanaitumia kanuni, lakini bado hawapati majibu mazuri. Hawa ni wale ambao wanatoa, halafu wanalazimisha kupata. Mfano ni pale mtu anapompa mtu mwingine kitu, halafu baadaye anamfuata kutaka kitu na kumkumbusha kwamba hata yeye alishampa kitu.

Haya siyo matumizi sahihi ya kanuni hii, usitoe halafu uje kudai. Wewe toa, halafu toa, kisha toa tena na baadaye usidai, bali omba.

Umenielewa rafiki. Toa, toa, toa, toa tena halafu omba, usidai. Omba au pendekeza na mpe mtu nafasi ya kuchagua mwenyewe kama atachukua hatua au la.

Kwa kufanya hivi watu watapata msukumo ndani yao ya kukupa kile ambacho umeomba au umependekeza, kwa sababu ndani ya nafsi zao wanajiona wana deni la kukulipa. Kumbuka hapa huwakumbushi chochote kwamba uliwapa, ila kwa kuwa umeshawapa sana, wao wenyewe watajikuta wakitaka kukupa pia.

Tumia kanuni hii vizuri rafiki yangu, inatoa matokeo bora sana mara zote. Toa, toa, toa na toa tena, kisha omba au pendekeza. Utapata chochote unachotaka, bila ya kulazimisha wengine. Iwe ni ongezeko la mshahara, kupanda cheo, kupata wateja zaidi na hata ushirikiano mwingine kwenye maisha yetu ya kila siku.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.