UKURASA WA 698; Maana Halisi Ya Uhuru Wa Kweli Kwenye Mafanikio…

By | November 28, 2016

Rafiki, hakuna mafanikio kwenye maisha yako kama huna uhuru wa kweli. Uhuru ni hitaji muhimu kwako ili kuweza kuwa na mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Na ninapozungumzia uhuru simaanishi ule uhuru wa kisiasa ambapo utaambiwa upo huru.

Kwenye mafanikio uhuru una wigo mpana zaidi, unaanzia ndani yako mwenyewe, kuweza kujitoa kwenye vifungo vya mawazo na kukupa uhuru wa kufikiria na kufanya yale ambayo ni muhimu kwako. Pia unakwenda kwenye ngazi ya familia, na kuweza kufanya kile ambacho ni muhimu kwako na siyo kile ambacho familia inalazimisha ufanye. Uhuru unakuwa muhimu zaidi kwenye jamii ambapo jamii ina matarajio fulani kwetu, tunapoweza kufanya yale ambayo ni muhimu kwetu bila ya kujali matarajio ya jamii.

Sasa leo nakupa maana ya ndani zaidi ya uhuru, ili uweze kuwa nao na uweze kuutumia kufikia mafanikio makubwa sana.

Uhuru unamaanisha kwamba yasiyowezekana ni mambo ambayo hayajajaribiwa kufanya. Kila utakapojaribu kufanya jambo jipya, watu watakuambia haiwezekani au utashindwa. Ukishakuwa na uhuru hutakubaliana nao kwa sababu unajua wanasema hivyo kwa sababu hawajawahi kumwona mtu mwingine akifanya, hivyo nakubali kuwa wa kwanza kufanya.

Uhuru unamaanisha ya kwamba changamoto kubwa tunazopitia ndiyo fursa kubwa kwetu kufanikiwa. Ukishakuwa huru hulalamikii tena changamoto, huzikimbii changamoto, badala yake unazikaribisha na kuzifanyia kazi, kwa sababu unajua kila changamoto ina fursa kubwa ndani yake.

Uhuru unamaanisha ya kwamba utakapofanya makubwa, wapo watu wengi watakaokukosoa na kukupinga. Ukishakuwa huru unajua kabisa kwamba wapo watu wengi watakaokupinga na kukukosoa siyo kwa sababu umefanya jambo lolote baya, ila tu kwa sababu unafanya makubwa ambayo hayajazoeleka. Kwa kuwa huru unalielewa hili na kulichukulia sehemu ya safari. Hukubali likurudishe nyuma.

Hii ndiyo maana halisi ya uhuru, kila siku unapopambana ili kufanikiwa, mambo hayo matatu yachukue kuwa sehemu yako, hata siku moja hutakwama au kukata tamaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.