UKURASA WA 703; Kazi Ya Maisha Yako Yote…

By | December 3, 2016

Kuna watu ambao wamekuwa wakifikiria pale walipo wao siyo sahihi, wanakuwa wanaangalia mahali pengine ambapo wanaweza kufanikiwa zaidi ya sasa. Lakini wanapopata kwingine, wanagundua hakuna tofauti kubwa na walipokuwa awali.

Unakuta mtu ameajiriwa sehemu fulani, lakini anaona pale hapamfai. Anaona sehemu nyingine ambayo ni bora zaidi kwake, anaacha kazi pale na kwenda sehemu hiyo nyingine. Mwanzoni anakuwa anafurahia kazi hiyo mpya, lakini siku zinavyokwenda anagundua hakuna tofauti kubwa.

Hata kwenye biashara pia, unakuta mtu anafanya biashara fulani, lakini anaiona haifai au haimpi anachotaka, anabadili na kufanya biashara nyingine, mwanzoni anaiona ni nzuri lakini kadiri siku zinavyokwenda anaona mambo ni yale yale.

Hili limekuwa linawatokea watu tena na tena na tena, yaani imekuwa kama mchezo wa kurudia na hivyo kusababisha watu kupoteza muda mwingi kwenye kuhama kwenye kazi au biashara moja na kwenda nyingine.

Sasa lipo suluhisho la changamoto hii,

Na suluhisho ni kuchagua kazi au biashara ya maisha yako, kazi ambayo utaifanya kwa maisha yako yote, ije mvua lije jua. Chagua kitu ambacho unataka kutoa mchango wako kwenye dunia hii, na kifanye kuwa kazi au biashara ya maisha yako yote.

Ukishachagua hivi unaacha sasa kukimbizana na fursa nyingi zinazoibuka kila siku, maana fursa huwa haziishi. Unaweka nguvu zako zote kwenye kuhakikisha unatoa mchango mkubwa kupitia unachofanya na hatimaye kupata kipato bora, sawasawa na mchango unaotoa kwa wengine.

Kufanya hivi siyo rahisi, kufanya hivi hakutatupa umaarufu hasa mwanzoni, lakini ni kitu muhimu kwetu, na tutawapata wale ambao wataona ni muhimu pia kwao.

Hivyo acha kufanya vile ambavyo vinaonekana ni maarufu kufanya, acha kukimbizana na fursa mpya kila siku, na badala yake chagua kazi au biashara ya maisha yako na ifanye, kila siku ukiongea juhudi na ubora mpaka mwisho wa maisha yako. Kwa kuchagua hivi, hakuna kitakachokuzuia kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.