UKURASA WA 704; Usidanganyike, Usiharakishwe…

By | December 4, 2016

Ukiangalia maamuzi ambayo watu wamekuwa wanafanya na yanawagharimu, lazima kutakuwa na moja kati ya hivi viwili, kudanganyika au kuharakishwa. Na matatizo haya yamekuwa yanatokana na watu ambao tunawaamini sana, lakini baadaye wanatuangusha.

Kwa mfano ni mara ngapi amekufuata ndugu au jamaa yako wa karibu na kukupa wazo zuri sana la biashara au mradi ambao mtaweza kufanya pamoja. Akakushawishi kwamba anaweza kusimamia vizuri maana yeye ana muda ila wewe huna. Ukaamini hilo na kumpa fedha, lakini mambo yakaenda tofauti na alivyoahidi. Akakosa umakini ambao unapelekea kupata hasara.

Mfano mwingine ni pale ambapo umekuwa unaharakishwa kwamba fursa hii ni ya kipekee na usipochukua hatua sasa utaikosa. Unajikuta unachukua hatua haraka na baadaye kuja kugundua umefanya makosa makubwa.

Kudanganyika.

Tumekuwa tunadanganyika sana na wale watu ambao tunawaamini, kwa kuwa tunawajua tunaamini watafanya vyema. Tunaweka matumaini yetu juu yao na mwishowe tunaumizwa.

Na hata wale ambao wana nia ya dhati ya kututapeli au kutudhulumu, wanaanza na kujenga imani zetu kwao. Wanaanza na matendo madogomadogo ambayo yatatufanya tuwaamini, baadaye wanatupiga matukio makubwa.

Hatua ya kuchukua hapa ni kuwaamini wale ambao unawaheshimu na kuwapenda na wanaokupenda pia, lakini inapokuja kwa mambo muhimu kwako, jisikilize wewe mwenyewe kwanza. Fanya upembuzi yakinifu ikiwa ni vyema kwako kuchukua hatua. Usikubali mahusiano mliyonayo yakuzibe macho na uache kuuona ukweli.

Kaharakishwa.

Watu wanapotaka kukutapeli au kukudhulumu, wanahakikisha hupati muda wa kufikiria kwa kina, wanajua ukifikiria vizuri utagundua wanachotaka kufanya, hivyo wanachofanya ni kukuharakisha wewe uchukue maamuzi. Wanakupa msukumo wa kuchukua maamuzi sasa, na kukutengenezea hali ya kukosa kitu kizuri iwapo hutachukua hatua sasa. Hali hii inakufanya ushindwe kufikiri sawasawa na kujikuta unafanya maamuzi ambayo siyo bora.

Hatua za kuchukua ni kujipa muda kwa jambo lolote kubwa unalotaka kufanya. Kamwe usikubali kuharakishwa kuchukua hatua, hata kama ni fursa kubwa na nzuri kiasi gani. Kama ni bora utaipata tu na kama utaikosa basi zipo fursa nyingine nzuri zaidi zinakuja. Jipe muda wa kufikiri vizuri na kujua ukweli kabla hujafanya maamuzi makubwa ya maisha yako. Fursa bora kwako inakuja kwa wakati sahihi kama utachukua muda na kuzijua fursa zako vizuri.

Usidanganyike, hasa na wale unaowaamini na pia usiharakishwe kufanya maamuzi yoyote kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.