UKURASA WA 708; Wazo Bora Pekee Halitoshi…

By | December 8, 2016

Watu wengi ambao wamekuwa wanataka kuingia kwenye biashara, wamekuwa wanaweka uzito sana kwenye kuwa na wazo bora la biashara. Wamekuwa wakitafuta wazo la kipekee na la tofauti ili kuweza kuanzisha biashara za kipekee. Hii ni hatua nzuri sana katika kuanza biashara. Ila tatizo linakuja pale mtu anapofikiri wazo bora pekee ndiyo kila kitu.

Pale ambapo watu wanaona wazo bora pekee ndiyo litawatoa, kwamba wazo bora litawafanya watu wawaunge mkono kwenye biashara zao, ndipo wanapopotea.

Wazo bora pekee halitoshi, wazo bora pekee siyo mafanikio ya biashara yako. Wazo bora ni wazo tu, na thamani yake siyo kubwa kwa sababu ni wazo.

Dunia ya sasa ina mawazo bora sana ya kibiashara. Yapo mawazo ukiyasikia unaona kabisa yanaweza kuleta mapinduzi makubwa sana kwenye maisha ya watu. Lakini linapokuwa wazo, bado halitoshi. Kitu kingine ni kwamba wazo tu kila mtu anaweza kuwa nalo, haihitaji nguvu kubwa kuja na wazo, tena bora na la kipekee.

Thamani kubwa ipo kwenye kufanyia kazi wazo bora, kwenye kuanza utekelezaji wa wazo hilo bora. Hapa ndipo penye kila kitu, kwa sababu unawapa watu ile thamani halisi ya wazo ulilokuwa nalo. Na pia hapa ni pagumu kwa sababu utakutana na changamoto halisi katika utekelezaji ambazo hukuziona wakati ukiwa na wazo.

Na ni wakati mgumu zaidi maana wapo ambao watakukataa na kukupinga, wapo ambao watatabiri kwamba hutafika mbali, na wapo wengi watakaokupa ushahidi kwamba wameona wengi wakianza kama wewe na wakapotea. Wengine hawatakuelewa kabisa, kwa kuwa unafanya kitu ambacho wao hawajazoea au hawajawahi kuona kikifanyika.

Hapa ndipo unatengeneza thamani halisi, kama ukiweza kuvuka yote hayo na ukasimamisha wazo lako, litakuletea mafanikio makubwa sana.

Hivyo rafiki, usiwapigie watu kelele za ubora wa wazo lako, badala yake waoneshe namna wazo hilo litakavyoweza kuleta mapinduzi kwa kulitekeleza. Hapa ndipo utakapoipata thamani halisi ya wazo lako bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.