Moja ya hatua muhimu unazopaswa kupiga kila siku ili kufanikiwa ni kuchukua jukumu kubwa na kuligawa kwenye majukumu madogo madogo. Kitu chochote kikubwa, huwa kinawatisha watu kufanya, kama ukiambiwa umle tembo, ni vigumu, lakini ukimkatakata tembo katika vipande vidogo vidogo unaweza kumla.
Tukija kwenye biashara, kuiangalia biashara kama biashara ni kitu kikubwa, inaweza kukutisha na kuona huiwezi. Biashara ina vitu vingi, uzalishe, uuze, utafute wateja, usimamie wafanyakazi, kuna wadau wengine, bado changamoto nyingine za kila siku. Kufikiria hivi unaweza kuona biashara huiwezi, maka ujipange sana.
Sasa kama kawaida yetu, tunamchukua tembo, tunamkata vipande na inakuwa rahisi kuliwa hata na mtoto mdogo, ili mradi tu awe na meno.
Sawa ninachomaanisha ni hiki, tunaweza kuielewa biashara na kuirahisisha katika maneno matatu tu. Maneno matatu tu na tukiweza kuyatahajudi haya kila siku basi tunaweza kuendesha biashara kubwa na zenye mafanikio.
Neno la kwanza; WATU.
Biashara ni watu, biashara inahitaji wateja ili iweze kuendelea kuwepo, na zaidi kabisa inahitaji watu wanaoiendesha. Hivyo unapofikiria biashara, anza kufikiria kuhusu watu.
Anza kufikiria kuhusu timu ambayo itakusaidia kuendesha na kukuza biashara yako. Fikiria namna watu hawa watahamasika ili kuweza kutoa huduma bora sana kwa wateja wa biashara yako.
Pia fikiria sana kuhusu wateja wa biashara yako, wana shida gani, wana changamoto zipi na mahitaji yao makubwa ni yapi ambayo unaweza kuyatimiza kupitia biashara hiyo.
Neno la pili; BIDHAA.
Lazima kuwepo na kitu cha thamani ambacho biashara inakitoa kwa wateja. Kitu hiki ndiyo bidhaa ya biashara, na kwa biashara za huduma, huduma hiyo ndiyo bidhaa ya biashara husika. Hakuna biashara kama hakuna bidhaa. Hata kama una timu nzuri na wapo wateja, wanahitaji bidhaa ili waweze kuenda na wewe.
Watu wana matatizo, changamoto na mahitaji yao ambayo wanataka yatimizwe. Yatimize hayo kwa kuwapa huduma na bidhaa nzuri sana na mtakuwa pamoja.
Neno la tatu; FAIDA.
Uwepo wa watu na bidhaa hautoshi kukamilisha biashara, kwa sababu ili biashara iweze kuendelea kuwepo, lazima uweze kuuza bidhaa kwa bei ya juu kuliko gharama zako za kuiandaa bidhaa na kuiuza. Kinyume na hapo utapata hasara na biashara haiwezi kuendelea kuwepo.
Faida ni eneo muhimu sana kwenye biashara yako, hii ndiyo inafanya biashara iendelee kuwa hai, watu walipwe, bidhaa zaidi ziandaliwe na watu wengi zaidi wafikiwe.
Haya ndiyo maneno matatu muhimu ya kutia juhudi kila siku kuhusu biashara. Mambo mengine yote kuhusu biashara yanaingia kwenye hayo matatu, mambo kama usimamizi, uzalishaji, matangazo na kadhalika.
Muhimu; mambo hayo matatu yanategemeana sana, kama mafiga ya jiko, huwezi kuendesha biashara kwa moja au mawili pekee, lazima yote matatu yawepo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK