UKURASA WA 716; Dunia Bado Ina Njaa…

By | December 16, 2016

Pamoja na wingi wa kila kitu kinachofanywa hapa duniani, dunia bado ina njaa kubwa sana ya kitu kimoja muhimu; kazi iliyo bora.

Pamoja na kwamba wapo watu wengi ambao wanafanya biashara, dunia bado ina njaa na bidhaa na huduma bora sana zinazoweza kuyafanya maisha ya watu kuwa bora zaidi.

Pamoja na wingi wa maarifa yanayopatikana bure kupitia mtandao wa intaneti, dunia bado ina njaa kubwa ya maarifa bora kabisa ya kuwawezesha watu kuchukua hatua na kuwa na maisha bora.

Pamoja na maendeleo makubwa ambayo yameshafanyika mpaka sasa, dunia bado ina njaa kubwa ya mapinduzi makubwa kwenye kila sekta.

Hivi ndivyo dunia inavyokwenda mara zote, na njaa hii ya dunia ndiyo imechochea maendeleo kupatikana kila siku. Mapinduzi makubwa yanafanyika na biashara zinazidi kuwa bora zaidi. Na hata wateja wananufaika zaidi na biashara zinazokuwa bora kila siku.

Kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo dunia inavyozidi kuwaendea watu wachache. Zamani kiwanda cha gari kilitengeneza gari la aina moja tu, na rangi moja tu. Kwa dhana kwamba hili ndiyo gari tunalotengeneza na rangi yetu ni hii, kama unataka nunua na kama hutaki basi kaendelee kuendesha farasi. Lakini sasa mambo yamebadilika, kampuni moja inazalisha magari ya aina tofauti na rangi tofauti, na hata ukitaka aina yako mwenyewe wapo tayari kukutengenezea.

SOMA; Siyo Kwamba Dunia Haina Huruma, Dunia Haina Muda Na Wewe.

Kwa nini ni muhimu sana sisi kujua hili?
Kwanza kuwa na matumaini kwa jambo lolote tunalotaka kufanya. Kama unataka kufanya kweli, hata kama kuna wengi wanaofanya, usitishike, kwa sababu bado dunia inataka kazi bora. Wengi watakuambia unapotea, lakini kama una msukumo wa kweli kutoka ndani yako, fanya, dunia bado ina njaa.

Pili kuboresha zaidi chochote ambacho unafanya sasa. Usije ukajidanganya hata siku moja kwamba tayari umeshafika kilele cha mafanikio. Ingekuwa hivyo tusingepata mashujaa wapya kila siku. Roger Banister alikuwa binadamu wa kwanza kuweka kukimbia maili moja chini ya dakika nne. Alishangiliwa sana kwa sababu hakuna mtu aliyewahi kufikiri kitu hicho kinawezekana, lakini unajua nini? Miezi sita baadaye watu watatu waliweza kukimbia maili moja chini ya dakika nne. Na sasa hivi hata vijana wadogo wanaweza kufanya hivyo. Chochote unachofanya, bado upo chini sana kulinganisha na uhitaji wa dunia.

Na mwisho kabisa, usiifikirie dunia nzima, bali mfikirie mtu mmoja, kisha watu wachache kisha kikundi cha watu. Hakuna unachoweza kufaya wewe ambacho dunia nzima itakukubali au itakuangalia wewe tu. Lakini yupo mtu na kipo kikundi cha watu ambacho kina imani fulani, na mitazamo fulani ambayo inaendana na kile unachofanya. Hawa wapo tayari kwenda na wewe kwenye kile ambacho umechagua kufanya.

Dunia bado ina njaa ya kazi bora, je ni eneo lipi umejipanga kutoa kazi ambayo ni bora kabisa?

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.