UKURASA WA 720; Kitu Pekee Unachomiliki Na Unachoweza Kubadili Kwenye Maisha Yako…

By | December 20, 2016

Kwenye maisha huwa tunafikiri tuna umiliki mkubwa wa vitu, mpaka pale ambapo vinapotutoka ndipo tunagundua ya kwamba tulikuwa tunajidanganya. Vitu vingi tunavyodhani tunavimiliki wala hatuna umiliki wa moja kwa moja kwenye maisha yetu.

Wapo walioamini kazi zao watadumu nazo mpaka walipoamka na kuambiwa huna kazi tena, ndipo walipoona ukweli kwamba kazi hazikuwa zao. Wapo walioamini kwamba biashara wanazofanya wanazimiliki moja kwa moja, mpaka pale mabadiliko yalipotokea na biashara zao kushindwa kuendelea ndipo walipojua kwamba hawakuwa na umiliki mkubwa wa biashara. Wapo waliofikiri wale watu walionao kwenye maisha yao wataendelea kuwa nao siku zote, mpaka pale mambo yalipobadilika na watu hao kutokuwepo tena ndipo wakajua watu wale hawakuwa wao milele.

Kazi, biashara na hata watu wanaotuzunguka kwenye maisha yetu, siyo mali zetu, hatuvimiliki moja kwa moja. Bali tumepata nafasi ya kuvitumia na kuzungukwa navyo. Hivyo tunahitaji kuvitumia vyema wakati tunavyo ili kuweza kuyafanya maisha yetu na ya wale wanaotuzunguka kuwa bora zaidi.

SOMA; Ikuingie, Ikumiliki….

Kitu pekee unachomiliki kwenye maisha yako ni TABIA yako. Hakuna anayeweza kukunyang’anya tabia yako, hakuna anayeweza kukufukuza kwenye tabia yako na hakuna anayeweza kukufilisi tabia yako.

Tabia yako ndiyo utambulisho wako kwenye hii dunia, baada ya yote unayotegemea kupita, tabia yako itabaki na hii ndiyo itakuwa sifa yako.

Tabia yako inaweza kukubeba zaidi kuliko kingine chochote unachotegemea. Kama tabia zako ni nzuri, hasa inapokuja kwenye kazi, hata kazi moja inapoisha hutakosa kazi nyingine. Kadhalika kwenye biashara na hata maisha kwa ujumla. Tabia ina nafasi kubwa sana kwenye maisha yako, kwa mambo gani unapata au kukosa.

Na habari njema zaidi ni kwamba tabia yako ni kitu ambacho wewe mwenyewe unaweza kukibadili. Hakuna anayeweza kukuzuia kubadili tabia yako, unaweza kuibadili vyovyote utakavyo.

SOMA; Je unamiliki biashara au biashara inakumiliki?

Kwa kuwa tabia ndiyo kitu pekee unachomiliki, na kwa kuwa unaweza kuibadili utakavyo, jijengee tabia ambayo itakuwa mtaji mkubwa kwako kufika popote unapotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.