UKURASA WA 726; Kilichojificha Nyuma Ya Hofu Ya Kufanya Mambo Makubwa….

By | December 26, 2016

Watu wengi wana mawazo bora sana ya namna ya kuboresha kazi zao, namna ya kuboresha biashara zao na maisha yao kwa ujumla. Karibu kila mtu anajua ni kitu gani cha tofauti anapaswa kufanya ili aweze kutoka pale alipo sasa na kufika mbali zaidi. Lakini cha kushangaza, sehemu kubwa ya watu hawafanyi chochote.

img-20161217-wa0002

Ukiangalia kwa juu utaona watu hawa wanazuiliwa na hofu, wamejawa na hofu na ndiyo maana wanashindwa kuchukua hatua. Licha ya kujua nini wanataka, wana hofu ya kuchukua hatua kwa sababu hawana uhakika kama kweli watapata kile wanachotaka. Hivi ndivyo unavyoona ukiangalia kwa juu juu.

Lakini ukizama ndani na kuchunguza zaidi utagundua ya kwamba hofu ni kitu cha nje tu. Kuna kitu kikubwa ambacho kimejificha ndani ya hofu, ambacho ndiyo hasa kinawazuia watu kuchukua hatua. Kitu hiki kinawafanya watu kukaa na mawazo mazuri miaka na miaka na hata kufa nayo bila ya kuyafanyia kazi.

Kitu hiki ni kukosolewa. Kukosolewa imekuwa sumu kubwa inayowafanya watu kushindwa kuchukua hatua. Hofu ya kushindwa pekee siyo kikwazo sana, kwa sababu kila mtu anajua kushindwa ni sehemu ya maisha. Hofu kubwa inatokana na kukosolewa, pale ambapo watu wataangalia kitu cha tofauti ulichofanya na kukushangaa kwa nini umefanya kitu cha hovyo kiasi hiko.

Pale unapopata picha ya kauli kama hizi kutoka kwa watu unaowaamini sana; “sikuamini kama ungeweza kufanya kitu cha ajabu kiasi hiki” au “nani kafanya kitu cha hovyo kiasi hiki” au “tulikuambia huwezi hukusikia” au “hiki ni kitu cha hovyo kabisa nimewahi kuona”.

Tunapofikiria kauli kama hizo tunachoka kabisa na kuona ni bora tuendelee kusubiri kwa sababu hatujawa tayari bado.

Ninachotaka kukuambia leo ni kwamba kama utafanya kazi au kitu kipya na watu wakakukosoa, basi furahia sana. Kwa sababu watu kukukosoa inamaanisha kwamba umefanya kitu ambacho watu wamejali, watu wamechukua muda wao kukipitia na hatimaye kuona mapungufu. Kingekuwa kitu cha hovyo kabisa wala hakuna ambaye angehangaika nacho. Usingepeta wa kukukosoa kwa sababu hakuna ambaye hata angepoteza muda wake na kitu hicho.

Kumbuka huwezi kumridhisha kila mtu, huwezi kukubalika na kila mtu. Wapo ambao watakukosoa kwa jambo lolote ambalo utafanya, lakini wapo wengi sana ambao watakubaliana na jambo hilo. Hivyo usiwanyime mambo mazuri watu kwa kuogopa kukosolewa na wachache.

Una njia bora ya kufanya kazi zako? Hebu anza kutumia njia hiyo na washirikishe wengine.

Una wazo la biashara ambayo unaweza kuifanya kwa utofauti? Hebu anza kulitekeleza.

Una ujumbe, maarifa au taarifa ambazo ungependa kuwashirikisha wengine kupitia mafunzo, maandiko na hata vitabu? Hebu kaa chini na toa mafunzo hayo.

Usihofie kukosolewa, hofia kukosa wa kukukosoa kabisa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.