UKURASA WA 747; Viungo Vitatu Vya Biashara Yenye Mafanikio…

By | January 16, 2017

Hakuna swali linaloulizwa na watu wengi kama biashara gani ambayo mtu afanye ili aweze kufanikiwa. Nimekuwa nasikia swali hili karibu kila siku kutoka kwa watu mbalimbali.

Mara zote nimekuwa nasema kila biashara inalipa, hivyo badala ya mtu kuuliza biashara gani inalipa, bali ajiulize yeye mwenyewe ni biashara gani anayoweza kufanya, ambayo inatoa thamani kwa wengine. Kupitia biashara hiyo anaweza kufanya makubwa.

Sasa jibu hili naona bado halitoshelezi, hivyo nimechimba ndani zaidi na nimekuja na viungo vikuu vitatu ambavyo kila biashara yenye mafanikio inavyo. Kama unataka kuanza biashara na hujui uanzie wapi, anza na hivi vitatu. Kama biashara yako ina changamoto, anza na vitu hivi vitatu.

Kitu cha kwanza ni kile ulichonacho au unachoweza kutoa.

Msingi wa biashara ni uwepo wa thamani, na thamani hii inaweza kuwa kwenye bidhaa au huduma ambazo wewe upo tayari kutoa.

Kitu cha pili ni uhitaji.

Je wapo watu ambao wanahitaji kile ambacho unacho au unatoa? Je wapo watu wenye uhitaji wa kweli na ambao wanatumia kile unachotoa? Uhitaji ndiyo unaokuletea wewe wateja.

Kitu cha tatu ni utayari wa kulipia.

Hapa ndipo maendeleo ya biashara yalipo. Je watu wapo tayari kulipia kile ambacho wewe unakitoa na wanakihitaji. Kwa sababu kuhitaji pekee haitoshi hiyo kuwa biashara, bali unataka watu ambao wapo tayari kulipa.

SOMA; Mafanikio Ya Wengine Ndiyo Mafanikio Yako…

Haya ni maeneo matatu muhimu ya kuijenga biashara yako, iwe una bidhaa au huduma ambayo utataka kuitoa kibiashara.

Kwa msingi huu unaweza kuingia kwenye biashara yoyote ile ambayo inakidhi vigezo hivyo vitatu na ukatengeneza biashara yenye faida.

Vipi kama huna vyote vitatu?

Vipi kama una kimoja au viwili? Je huwezi kuingia kwenye biashara au kukuza biashara yako? Jibu ni unaweza.

Kama una bidhaa au huduma na huna wateja, basi unaweza kutafuta wateja wa bidhaa au huduma hiyo, kuwaikia kule walipo na kuhakikisha wanajua kuhusu biashara yako.

Kama una watu wanaokufuata na kukukubali lakini huna bidhaa ya kuwauzia, unaweza kushirikiana na mwenye bidhaa na kisha ukanufaika kupitia faida ambayo inapatikana.

Na kama una bidhaa au huduma na una watu lakini hawapo tayari kulipia, unaweza kutafuta mtu ambaye yupo tayari kuwalipia ili wapate kile unachotaka kuwapa. Na hapa ndipo unapohitaji kuwa na wadhamini.

Kwa vyovyote vile, angalia ni wapi umekwama sasa na anzia hapo kusonga mbele.

Kama nia yako ni kuanzisha biashara, au kukuza biashara yako, basi una kila fursa ya kufanya hivyo, ondokana na hali ya kujiona hujawa tayari na anza kuchukua hatua sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.