UKURASA WA 748; Kuridhika Na Pale Ulipo Sasa…

By | January 17, 2017

Kama kuna kitu kimoja ambacho hakibadiliki basi ni mabadiliko ya dunia. Hata iweje, dunia itaendelea kubadilika, kila siku. Hivyo basi hatua bora kwa sisi kuchukua ni kubadilika kadiri dunia inavyobadilika. Na kama ukiwa mjanja unaweza kubadilika kabla hata dunia haijabadilika.

Watu wengi huwa wanaanzia chini, wanapambana sana kufanikiwa, wanayaonja mafanikio kidogo halafu wanapotea kabisa, yaani wanarudi chini badala ya kwenda mbele zaidi.

Hali hii imekuwa ikisababishwa sana na kuridhika na kuzoea pale ambapo mtu anakuwa amefika. Mtu anapoanza kupata mafanikio, anasahau juhudi kubwa zilihitajika kumfikisha pale na kuanza kufikiri labda yeye ni mjanja kuliko wengine, au ana bahati zaidi ya wengine. Anaacha kuweka zile juhudi na mwishowe anaanza kuanguka.

SOMA; Jinsi Ya Kutumia KANUNI YA DHAHABU Kupata Mafanikio Makubwa Kwenye Maisha Yetu.

Hivyo leo nataka tukumbushane wana mafanikio ya kwamba juhudi hazina mwisho, iwe umefika au hujafika ulikopanga kufika, unahitaji kuendelea kuweka juhudi zaidi.

Na ndiyo maana msingi wa maisha yetu ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA. Hivi ni vitu ambavyo unapaswa kuvifanya kila siku, iwe tayari umefanikiwa au bado hujafanikiwa.

Usijidanganye kwamba ukishafanikiwa basi huhitaji tena nidhamu, unachopaswa kujua ni kwamba unahitaji nidhamu zaidi ukishafanikiwa kuliko hata wakati hujafanikiwa.

Ukichukulia mkaisha kama kupanda ngazi, ukiwa chini ya ngazi huhitaji umakini mkubwa, kwa sababu huwezi kuanguka au ukianguka huwezi kuumia. Lakini kadiri unavyopanda ngazi kwenda juu, ndivyo unavyohitaji umakini mkubwa kwa sababu ukianguka, utakwenda mbali sana na pia utaumia sana kutokana na urefu ambao umeshapanda.

Hivyo kwa maisha yako yote, NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA vinapaswa kuongezeka zaidi kadiri unavyofanikiwa. Mafanikio yasikufanye usahau misingi hii na mwishowe uanguke vibaya. Usiridhike na kujisahau kwa mafanikio yoyote ambayo umepata, jua mbele yako bado kuna kazi kubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.