UKURASA WA 750; Tengeneza Uhalisia Unaoutaka Wewe…

By | January 19, 2017

Kila mmoja wetu ana uhalisia wake wa maisha ambao anauishi. Kuna mambo unayafanya au kutoyafanya kwa sababu tu ya uhalisia wako, kwa sababu ya unavyochukulia maisha yako. Uhalisia wako unaweza kuwa mzuri au mbaya kwako.

Kwa sehemu kubwa, uhalisia ulionao hujautengeneza wewe mwenyewe, bali umepewa kwenye jamii uliyokulia, kutoka kwa wale ambao wanakuzunguka. Ulizaliwa na kukuta watu wanafanya vitu fulani na wewe umekuwa unafanya. Au umeingia kwenye biashara na kukuta watu wanafanya vitu fulani kwa njia fulani na wewe ukafanya hivyo.

SOMA; Hiki Ndio Unachohitaji Ili Kugeuza Ndoto Yako Kuwa Uhalisia.

Mara nyingi watu wanafanya vitu ambavyo hawajui kwa nini wanafanya, lakini vinawaletea majibu. Hii ina maana kwamba haijalishi kama uhalisia unaoishi ni sahihi au la, utakuletea yale majibu unayotarajia. Sasa hapa ndipo pazuri katika kutengeneza yale maisha unayoyataka wewe mwenyewe.

Unaweza kutengeneza maisha yako kwa kuanza na kutengeneza uhalisia wa maisha yako. Anza kwa kujipa uhalisia wa mambo gani unaweza kuyafanya, mambo gani ni muhimu kwako na vipaumbele vyako vikoje.

Unaweza kutengeneza uhalisia wako kwa kuanza na picha kubwa ya maisha yako, kwa kuwa na maono ambayo unataka kuyafikia. Baada ya hapo unahitaji kuangalia njia ambayo itakufikisha kwenye maono hayo, mambo unayohitaji kufanya ili kufika pale. Halafu unatengeneza maisha yanayoendana na maono uliyonayo, na huu unakuwa uhalisia wako mpya.

Ukijichunguza uhalisia unaoishi sasa umetokana na maono ya wengine, hivyo unajikuta unaweka juhudi kubwa lakini hazikunufaishi sana wewe.

Pia uhalisia ambao umekuwa unaishi unaweza kuwa umekuwekea ukomo na vikwazo vingi ambavyo havina hata maana. Labda kuna uhalisia unaoishi kwamba watu kama wewe huwa hawafanyi vitu vya aina fulani. Labda wasomi wa ngazi yako hawawezi kufanya aina fulani ya biashara. Swali ni nani aliyesema hivyo? Ukianza kuhoji hapo utaweza kujitengenezea uhalisia mpya unaoendana na maisha unayoyataka wewe.

Kama umechagua maisha ya mafanikio, basi usikubali kufanya au kuacha kufanya kitu kwa sababu tu wengine wanafanya au hawafanyi. Tengeneza uhalisia wako mwenyewe, ambao utakusukuma kufanya au kutokufanya vitu kutokana na maono yako ya maisha uliyonayo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.