UKURASA WA 753; Zawadi Inapogeuka Kuwa Adhabu…

By | January 22, 2017

Saikolojia ya binadamu inaendeshwa na vitu viwili vikuu, raha na maumivu. Kila tunachofanya ni kwa sababu tunapata raha kwenye kulifanya, au tunapata maumivu tusipolifanya.

Saikolojia hii pia imekuwa inatumika kutengeneza tabia fulani ambazo ni nzuri kwenye jamii. Na hapa vimekuwa vinatumika vitu viwili muhimu; zawadi na adhabu.

Mtu anapofanya kitu kizuri anapewa zawadi na anafurahi, hii inampelekea kurudia zaidi kile ambacho amefanya na hivyo kutengeneza tabia nzuri.

Mtu anapofanya kitu kibaya anaadhibiwa na hii inamuumiza kwa maumivu anayopata harudii tena kufanya kile alichokifanya.

Hivi ndivyo tulivyolelewa tangu tukiwa watoto na ndivyo jamii inavyotupeleka. Zawadi na adhabu.

Lakini siyo kila zawadi inakuwa zawadi, mara nyingi zawadi inageuka kuwa adhabu, hasa kwa yule anayetoa zawadi hiyo.

Kwa mfano mtu anapopewa zawadi kwa kufanya kitu fulani, atapenda kupata zawadi hiyo zaidi na zaidi. Na ikiwa atashindwa kufanya kitu kile kinachopelekea kupata zawadi, anaweza kutafuta njia ya kudanganya ili apate zawadi. Na hii inamuumiza yule ambaye anatoa zawadi.

SOMA; Zawadi Kubwa Kabisa Unayoweza Kumpa Mteja Wako.

Wakati mwingine mtu anaweza kuwa hakufanya kitu hiko vizuri, ila alionekana anafanya vizuri. Au ni kitu hicho kimoja tu amefanya vizuri, vingine amekuwa anafanya vibaya. Sasa anapopewa zawadi, wale wanaomjua kweli kwamba huwa anafanya vitu vibaya pia, watasukumwa na wao kuficha yale mabaya yao yasionekane, japo wanaendelea kuyafanya ili nao wapate zawadi.

Wakati mwingine mtu ambaye siyo sahihi anaweza kupewa zawadi na anayestahili asipewe, hili linamvunja moyo yule aliyestahili na mwishowe kuwafanya wengine watafuta njia zisizo sahihi za kupata zawadi ile.

Na mwisho kabisa mmoja anapopewa zawadi anaweza kugeuka adui kwa wengine ambao hawajapata zawadi ile.

Adhabu pia inaweza kuleta matokeo tofauti na yanayotegemewa kama tulivyoona kwenye zawadi hapo, hasa pale mtu ambaye siyo sahihi anapoadhibiwa.

Haya yote ni muhimu kwetu sisi wanamafanikio kwa sababu tuna watu ambao wao chini yetu na tungependa kurekebisha au kujenga tabia zao kwa zawadi na adhabu. Watoto wetu, wenza wetu, ndugu zetu na hata wafanyakazi wetu, tunahitaji kuwa makini sana kwenye utoaji wa zawadi na adhabu, isije kugeuka mzigo kwetu.

Kwa kifupi, tunahitaji kuwa na njia bora ya kujenga na kurekebisha tabia zaidi ya zawadi na adhabu. Na njia hiyo ni kujenga ushirikiano na kufanya kile mnachofanya kama timu moja, ambapo mmoja akikosea mmekosea wote na mmoja akifanya vizuri mmefanya vizuri wote. Kwa njia hii mnaweza kurekebishana vizuri na kufanya makubwa kwa pamoja.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.