UKURASA WA 756; Una Nini Hapo Ulipo Sasa?

By | January 25, 2017

Watu wengi wana ndoto kubwa za maisha yao, lakini wachache ndiyo wanaoweza kuzifikia ndoto hizo.

Kuna usemi kwamba wapo wanaoota ndoto halafu wanarudi kulala, na wapo wanaoota ndoto halafu wanaamka mapema na kwenda kuzifanyia kazi.

Zipo sababu nyingi zinazowatofautisha wale wanaofikia ndoto zao na wanaoshindwa, ila moja kubwa ni namna mtu anavyoanzia pale alipo sasa. Hii ndiyo tofauti kubwa kabisa, imewanufaisha wengi na kuwarudisha nyuma wengi pia.

Wengi wanapokuwa na ndoto kubwa, huwa wanafikiria makubwa sana, kitu ambacho ni kizuri, ila tatizo wanasahau kwamba hawawezi kufika popote wanapotaka kufika, bila ya kuanzia pale walipo sasa. Wanasahau kwamba hawawezi kuwa mabilionea, kama hawawezi kuitumia vizuri shilingi elfu moja waliyonayo sasa.

Hivyo rafiki yangu, kwa ndoto kubwa ambayo unayo, na ninajua unayo, angalia pale ulipo sasa. Unawezaje kupatumia hapo ulipo sasa kufika mbali zaidi ya hapo ulipo? Ni muhimu sana kufikiri hivi kwa sababu hapo ulipo sasa ni muhimu mno. Kuna vitu vimekufanya uendelee kuwa hapo, na hivyo kupiga hatua lazima uanze kutoka hapo. Na  hutatoka kimuujiza bali kwa kupatumia vizuri.

SOMA; Kama Unachagua Mwenyewe, Kwa Nini Uchague Hovyo?

Njia nyingine tofauti ya kufikiri ambayo haianzii na hapo ulipo sasa ni ya kukupotezea muda, bila ya kujali ndoto yako ni kubwa kiasi gani na una hamasa kiasi gani. Lazima uanzie hapo ulipo sasa.

Sasa unapoanzia hapo ulipo sasa, unaanza na hicho ulichonacho sasa. Kipi unacho sasa kwa hapo ulipo? Hicho ndiyo unaweza kukitumia kupiga hatua zaidi.

Angalia kila ulichonacho, kuanzia tabia zako, vipaji vyako, uwezo wako, nafasi yako kijamii, ndugu jamaa na marafiki, kazi au biashara yako, watu fulani wanaokuamini na hata changamoto au matatizo uliyonayo sasa. Kila ulichonacho, iwe ni kizuri au kibaya, unaweza kukitumia kutoka hapo ulipo na kuzifikia ndoto zako.

Kizuri kitakupa hamasa ya kufanya zaidi na kibaya kitakupa hasira ya kuondoka hapo ulipo.

Ni lazima uanzie hapo ulipo, kwa kile ulichonacho, lakini muda wote ukiwa na picha kubwa ya ndoto yako kwenye akili yako, ili chochote unachofanya, kiwe kinakusogeza karibu zaidi na ndoto yako.

Leo kaa chini na orodhesha kila ulichonacho, kuanzia tabia zako binafsi, vipaji na uwezo, kisha vitu unavyomiliki, halafu watu wanaokuzunguka na hata shughuli unazofanya. Kisha viangalie namna gani vinaweza kukufikisha kwenye ndoto kubwa ya maisha yako. Hii ndiyo hatua muhimu na nzuri sana ya kuanzia, maana hakuna mtu atakayetoka popote alipo kuja kukubeba wewe na kukupeleka kwenye ndoto yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.