UKURASA WA 763; Hakikisha Watu Wanafanya Kile Wanachopaswa Kufanya….

By | February 1, 2017

Kama wapo watu wanaofanya kazi chini yako, labda kwenye ajira una watu ambao wewe unawasimamia, au kwenye kazi shughuli zako umeajiri watu ambao wanakusaidia, basi moja ya majukumu yako ni kuhakikisha watu wanafanya kile wanachopaswa kufanya.

Unahitaji kujua kwa karibu na hata kuwakumbusha kuhusu majukumu yao, kuona maendeleo yao na hili unapaswa kufanya mara kwa mara, na inakuwa bora zaidi kama unaweza kufanya kila siku.

Unahitaji kufanya hivi siyo kwa sababu unataka kuwatawala, bali kwa sababu unataka kuhakikisha wote mnakwenda pamoja, unataka kuhakikisha hakuna mahali ambapo wamekwama na unataka kuwasifia kwa kazi nzuri wanayoifanya.

SOMA; Wakati Sahihi Wa Kufanya Mabadiliko Ni Huu…

Kwa kufuatilia watu kwenye kile wanachofanya, inaonesha ni kwa namna gani upo makini na kile unachotaka kifanyike, hivyo watu hao nao wanakuwa makini na kazi zao pia. Umewahi kumwambia mtu kitu cha kufanya, halafu hukumwuliza tena kama amefanya na yeye akaacha kufanya? Siyo kwamba amekudharau, ila ameona hakina umuhimu na hivyo naye akasahau kukifanya.

Chochote unachotaka kutoka kwa watu, hakikisha unakifuatilia kwa karibu, hakikisha watu wanajua utauliza, watu wanajua utafuatilia na hivyo watajiandaa vizuri, watakuwa na majibu na watakua na cha kukuonesha utakapohitaji kuoneshwa.

Zipo changamoto nyingi za watu kuanzisha biashara, kutokana na kukosa muda wa kusimamia basi wanawaachia wengine, wanasahau kabisa kuhusu biashara hizo kwa sababu kuna watu wanazisimamia vizuri. Mambo huwa yanaenda vizuri mwanzoni mpaka pale changamoto zinapoanza, na huwa zinaanza pale mtu anapokuwa amezoea anachofanya na kujisahau kwamba anapaswa kutoa ripoti kwako. Hapo anaanza kufanya maamuzi ambayo yataathiri biashara yako.

Epusha hilo kutokea kwa kuhakikisha kila siku unajua kila kinachoendelea kwenye biashara yako, au kazi yako. Hakikisha unajua watu wanakwama wapi na wasaidie kuweza kusonga mbele zaidi. Kwa sababu mara nyingi watu wanapokwama, huwa wanatafuta njia rahisi kwao, sasa kama wewe utakuwa karibu, utaweza kuwasaidia kufuata njia sahihi na hivyo kupata majibu mazuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.