Watu wengi wamezikosa fursa nzuri ambazo walikuwa wanazitaka kwa kushindwa kuuliza au kuomba kile ambacho walitaka kupata kwa wengine. Labda mtu anamwona mtu ambaye angefaa kuwa mteja wake, lakini anahofia kumuuliza kama angependa kununua bidhaa anayotaka kununua. Au mtu angependa kupata ushirikiano au mchango wa wengine, lakini anaogopa kuwaomba mchango ule anaotaka.
Kuogopa huku kunatokana na hofu ya kukataliwa. Moja ya vitu ambavyo binadamu hatupendi ni kukataliwa, hatupeni mtu atuambie HAPANA, hatupendi mtu atuambie HAIWEZEKANI, hivyo tunaepuka mazingira yoyote yanayoweza kupelekea kuleta hali hizo.
Pale ambapo tunaona mtu atatuambia hapana au haiwezekani, tunahofia kuuliza au kuomba. Lakini tunasahau ya kwamba kwa kutokuuliza au kuomba bado pia hatujapata. Yaani ni sawa na sisi wenyewe ndiyo tumejiambia HAPANA au HAIWEZEKANI. Tumeogopa kuambiwa na wengine, lakini tunakubali kujiambia sisi wenyewe.
SOMA; Saikolojia Ya Kuuza, Uza Bei Ghali Kabla Ya Rahisi.
Leo nakwenda kukushirikisha njia ya kukuwezesha kuondokana na hofu hii ya kushindwa kuuliza au kuomba unachotaka. Leo nakwenda kukushirikisha siri ya kuweza kuwa na ujasiri wa kuomba au kuuliza chochote kwa mtu yeyote.
Siri yenyewe ni hii, mpe mtu ruhusa ya kusema HAPANA, mpe ruhusa ya kusema HAIWEZEKANI. Unachofanya unachukua hatua ya kuuliza au kuomba, ukiwa umeshakubaliana na nafsi yako kwamba unaweza kuambiwa hapana. Pia unakubaliana na nafsi yako kwamba kuambiwa hapana siyo mwisho wa dunia, wala haimaanishi wewe hufai, bali inamaanisha mtu yule hahitaji kile ulichomwambia au hujamwelewesha vizuri.
Kwa dhana hii pia unakubaliana na nafsi yako kwamba kama usipouliza kabisa, jibu ni hapana, na hutapata unachotaka kwa njia yoyote ile. Hii ina maana utakuwa umejiambia hapana mwenyewe. Lakini ukiuliza, jibu linaweza kuwa HAPANA, kama ambavyo ipo kabla hujauliza, na hivyo hakuna kilichobadilika, au jibu linaweza kuwa NDIYO na ukapata kile unachotaka kupata.
Wakati wowote unataka kuomba au kuuliza kitu na unapata hofu ya kuambiwa hapana, uliza ili usikie hiyo hapana vizuri. Usikubali kujiambia hapana wewe mwenyewe, isikie kutoka kwa yule ambaye unataka kumwambia kitu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK