UKURASA WA 781; Kujilisha Upepo…

By | February 19, 2017

Tatizo la kujilisha upepo ni kwamba huwezi kushiba, hata tumbo likijaa upepo, haitachukua muda utatoka na utaendelea kuwa na njaa yako kama ilivyokuwa awali.

Wapo watu ambao wameamua kuyaishi maisha yao kwa mtindo huu wa kujilisha upepo. Na upepo ambao wamekuwa wanajilisha ni matumaini ya uongo juu ya maisha ya furaha.

IMG-20170218-WA0001

Huwa inaanza hivi; mtu anafikiri ya kwamba pale alipo sasa hana furaha na wala maisha yake hayafai, na kujiambia ya kwamba iwapo tu atapata kitu fulani, basi maisha yake yatakuwa ya furaha sana. Anaanza kusakanya kile alichojiambia ndiyo kitamletea furaha, anaahirisha maisha mengine akiamini akishapata hicho tu, basi ni raha milele. Anakipata na haichukui muda, anagundua kwamba hali yake bado ipo vile vile ilivyokuwa mwanzo, kabla hata hajapata alichokuwa anatafuta.

SOMA; Usichukue Ushauri Kwa Mtu Wa Aina Hii…

Anafikiri labda kuna hatua ambayo bado hajafikia ndiyo maana bado hapati furaha aliyotazamia kupata. Anaendelea kujilisha upepo na kuendelea kuwa vile alivyo.

Ninachotaka kukukumbusha wewe rafiki yangu ni kwamba, chagua kwanza maisha ya furaha, kabla hujawa na chochote kile unachofikiria lazima uwe nacho ndiyo uwe na furaha. Unahitaji kuanzia hapo ulipo sasa ndiyo uweze kufika popote unapotaka kwenda, na siyo kuanzia sehemu ya kufikirika ili kufika sehemu nyingine ya kufikirika.

Maisha yako ndiyo hayo uliyonayo sasa, ukiacha fedha na mali unazoweza kuchuma kutokana na juhudi zako, hakuna kikubwa kinachokwenda kubadilika kwako. Namna unavyoiona dunia sasa ndivyo utakavyoendelea kuiona, namna unavyoyachukulia maisha sasa ndivyo utakavyoendelea kuyachukulia.

Hivyo chagua kuanzia hapo ulipo sasa, ukiwa na mtazamo sahihi juu ya maisha na utaendelea kuwa bora zaidi.

Muhimu; mafanikio ni matokeo ya juhudi zetu, lakini hayatabadili hali yetu ya furaha au mtazamo tulionao juu ya maisha yetu na maisha kwa ujumla. Anza kwa mtazamo sahihi na utakuwa na maisha sahihi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.