UKURASA WA 786; Mtu Mwenye Bahati Mbaya Na Mtu Mwenye Kisirani…

By | February 24, 2017

Mtu mwenye bahati mbaya sana kwenye hii dunia, ni yule ambaye hajajua ni nini anataka kwenye maisha yake, hajajua ndoto yake kubwa ni ipi na hajui kipi cha kipekee anachoweza kuchangia hapa duniani. Hivyo anajikuta anafanya kile ambacho wengine wanafanya, hathubutu kufanya makubwa wala ya kipekee, kwa sababu hajui makubwa anayotaka, au hawezi kuhimili kupingwa na wengine.

IMG-20170217-WA0003

Mtu mwenye bahati mbaya zaidi, au tuseme mwenye kisirani, ni yule ambaye anajua nini anataka kwenye maisha yake, anaijua ndoto yake kubwa, lakini hajaanza kuifanyia kazi. Kila anapofikiria kuanza anajiona hayupo tayari, kila akipanga kuanza kunakuwa na kikwazo kinamfanya aendelee kusubiri. Huyu ni mtu anayeishi maisha ya kujinyanyasa kwa sababu anajua kuna makubwa zaidi mbele, lakini hayaendei.

Nasema huyu ni mtu mwenye kisirani, na usichukie kama wewe ni mmoja wao, kwa sababu anaona lakini hapati kile anachoona. Unajua yule anayeona kitu kizuri halafu hakipati, anaumia sana kuliko yule ambaye haoni kabisa. Sasa huyu ambaye ana ndoto kubwa, lakini haifanyii kazi, anaumia kila siku, kwa sababu kadiri maisha yake yanapokuwa magumu, anaona namna gani ndoto yake ingemsaidia kama angekuwa ameifikia.

Cha kushangaza sasa, hakuna hatua anayochukua, kwa sababu ana sababu zinazomfanya asiweze kuanza sasa.

SOMA; Jinsi Ya Kuongeza Bahati Yako Ya Kufanikiwa…

Kama ambavyo unanijua rafiki yangu, mimi sijali sababu zako, hata ziwe zina ukweli kiasi gani, mimi ninachojali ni wewe uanze kufanya, ANZA KUFANYA, hata kama ni kwa hatua ndogo sana. Yaani kwa msisitizo nasema JUST DO IT, ni hivyo tu, hakuna namna nyingine.

Muda unaochagua kupoteza hapa duniani ni ule muda ambao unafanya mambo ambayo hayaendani na ndoto yako. Unaiweka ndoto yako pembeni na kukazana na mambo mengine. Hata kama mambo hayo ni muhimu kwa sasa, lakini ndoto yako ina umuhimu zaidi. Hivyo kamwe usiiweke kando, hakikisha unaifanyia kazi kila siku. Hakikisha ipo hatua, hata kama ni ndogo sana unapiga kila siku kuelekea kwenye ndoto yako.

Usipoteze muda rafiki yangu, hebu anza kupiga hatua leo kuelekea kwenye ndoto yako, na kesho piga hatua nyingine tena, kidogo kidogo miaka michache ijayo, utakuwa mbali kuliko ulivyo sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.