UKURASA WA 787; Epuka Kaburi Hili La Upya…

By | February 25, 2017

Nimeona kaburi moja ambalo linazika ndoto za wengi, kaburi hilo ni upya.

Wapo watu ambao wanapanga kufanya kitu, lakini kabla hawajaanza au pale tu wanapoanza, inajitokeza fursa mpya, ambayo inaonekana ni bora zaidi. Wanaacha kile walichotaka kufanya au walichokuwa wameanza, wanakimbiza kile kipya. Wakianza tena wanaona kingine kipya zaidi. Wanakimbizana na upya huu mpaka siku wanajikuta muda umekwenda na hakuna kikubwa walichofanya.

IMG-20170217-WA0003

Nataka nikuambie rafiki yangu, nimechukua muda wangu kujifunza, na bado naendelea kujifunza zaidi kutoka kwa wengi waliopita hapa duniani, miaka 500 mpaka 2000 iliyopita, na kikubwa ninachoona ni hiki, hakuna kitu kipya kabisa ambacho kinatokea kwa sasa. Kinachotokea sasa ni njia bora zaidi za kufanya mambo, na wala siyo upya wa mambo.

Kila tunachofanya sasa, kimekuwa kinafanywa miaka mingi iliyopita, kinachobadilika ni njia za kufanya. Hata wizi na utapeli uliopo sasa, siyo mpya, umekuwepo enzi na enzi, sasa hivi kilichobadilika ni njia tu.

Kwenye mafanikio pia, ya kazi, biashara na maisha kwa ujumla, hakuna kitu kipya kabisa, mambo ni yale yale, ila kuna njia bora zaidi za kufanya.

SOMA; Epuka Vitu Hivi Vinavyoua Ubunifu Wako….

Hivyo rafiki yangu, usipoteze muda kwa kuhama hama mambo unayofanya, chagua kimoja ambacho unataka kweli kukifanya, kifanye kwa moyo wako wote. Kazi yako kila siku iwe ni kuangalia njia bora zaidi za kuboresha, kujifunza zaidi kuhusu kitu hicho na kuwa bora zaidi.

Mtu akikuambia unachofanya sasa hivi siyo, fanya hiki kipya achana naye, huenda hajui anachosema au anataka kukutapeli. Kwa vyovyote vile usimsikilize.

Wengi wamekuwa wanaacha mifumo mizuri na inayofanya kazi, na kukimbilia mifumo inayoonekana mipya na isiyo sahihi. Kwa mfano msingi wa biashara ni huu; toa thamani kwa wale ambao wanaitaka, na wao watakuwa tayari kulipia. Hilo haliwezi kubadilika milele. Sasa watakuja watu na kukuambia sijui ukikusanya hela, na kuwaambia wengine watano, wewe unapata mara tano zaidi. Na wengi watakimbilia hilo, mwishowe wanatapeliwa. Mtu anapokuambia kuna njia rahisi ya kupata fedha, muulize ni thamani gani unatoa, kama hawezi kukujibu bila ya shaka, achana naye mara moja.

Nimalize rafiki, kwa kukusisitiza sana ya kwamba, mafanikio hayaji kwa kukimbiza upya, bali yanakuja kwa kuchagua kile unataka kufanya, kukifanya kwa muda mrefu na kuwa bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.