UKURASA WA 793; Sikio La Kufa….

By | March 3, 2017

Kuna sehemu ambapo nimekuwa napata huduma zangu za kimtandao, nimekuwa nafanya nao kazi kwa karibu miaka miwili sasa. Lakini miezi ya hivi karibuni, huduma zao zimekuwa siyo nzuri kama za awali, nimekuwa nakosa kile ninachokitaka hasa. Nimekuwa nawaeleza wazi kipi nataka na jinsi ninavyokikosa, wananipa ahadi wanafanyia kazi. Lakini baada ya siku chache tatizo linarudi pale pale. Hivyo nimeamua kuchukua hatua ya kuachana nao, bila hata ya kuwaambia na kutafuta huduma bora zaidi.

IMG-20170218-WA0000

Waswahili wanasema sikio la kufa halisikii dawa, kauli hii ina sehemu kubwa sana ya uhalisia, kuna wengi ambao wanakosea na hawapo tayari kujirekebisha,

Sasa wewe rafiki yangu, usiwe sikio la kufa, hasa kwenye biashara. Kwa sababu kama ambavyo nimekuwa nakuambia mara kwa mara, demokrasia ya kweli ipo kwenye biashara. Kama mtu hafurahishwi na huduma anazopata kwako, anaweza hata asikuambie, badala yake anaenda kule anakopata huduma bora zaidi.

SOMA; Una Mdomo Mmoja Na Masikio Mawili Kwa Sababu Hii Kubwa.

Hivyo unahitaji kuwa macho sana na biashara yako na wateja wako pia, angalia ni vitu gani hasa wanataka na wanavipataje kwenye biashara yako. Angalia vitu gani wanaulizia ila hawapati, na angalia vitu gani walitarajia kupata lakini hawapati. Ukishapata taarifa hizi, zifanyie kazi mara moja, kabla mteja hajapata sehemu nyingine inayomridhisha zaidi.

Bill Gates aliwahi kusema, mteja ambaye hajaridhishwa ni fursa kubwa kwako kujifunza na kuboresha biashara yako. Hivyo unahitaji kujua hilo na kuchukua hatua mara moja. Kwa sababu siyo kujua tu kwamba mteja hajaridhishwa ndiyo muhimu, bali unahitaji kuchukua hatua mara moja.

Dunia ya sasa, kila kitu kinapatikana kwa haraka, na hivyo uvumilivu wa watu umepungua sana. Mtu kuendelea kusubiri hawezi, anataka kitu na anakitaka sasa. Asipokipata kwako ataangalia wapi pengine anaweza kukipata.

Ukichagua kuwa sikio la kufa, husikii yale wateja wako wanasema kuhusu biashara yako utabaki wewe na biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.