UKURASA WA 796; Changamoto Kuu Ya Sasa Ni Subira….

By | March 6, 2017

Tunaishi kwenye ulimwengu ambao mapinduzi ya sayansi na teknolojia yamebadili maisha kwa kiasi kikubwa mno. Ujio wa simu janja (smartphone), mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii, umebadili kila eneo la maisha yetu. Kuanzia kwenye kazi, biashara na hata maisha yetu ya kawaida, mambo siyo tena kama zamani.

IMG-20170227-WA0003

Kwa mfano zamani kabla ya ujio wa simu, mtu alikuwa akitaka kumwona mtu, ilibidi aende pale anapopatikana kwa muda husika, bila ya kujua kama yupo au la. Na akifika pale akakuta hayupo, basi ilimbidi asubiri, bila hata ya kujua atarudi saa ngapi. Lakini sasa hivi, kabla hujaenda kumfuata mtu unampigia simu na kujua yupo wapi, na usipomkuta mtawasiliana kwa simu ili hata kama ni kusubiri ujue unasubiri kwa muda gani.

Huu ni mfano mmoja, lakini mabadiliko haya yamegusa kila eneo. Kwenye biashara, zamani wafanyabiashara walikuwa wachache, hivyo watu walijipanga mstari kusubiri kuhudumiwa. Na hapo pia wafanyabiashara wakawa na mazoea, waliweza kuwasubirisha watu hata kama hakuna la msingi wanafanya. Kwa mfano mtu anaweza kuwa anaongea na simu na kumwambia mteja asubiri.

SOMA; Changamoto Za Kuondoka Kwenye Vifungo Vya Maisha Na Kupata Uhuru Wa Maisha.

Sasa hivi ni vigumu kukuta hali kama hiyo, wateja hawana subira hata kidogo, kama ilivyo kwenye hali nyingine za watu. Mteja akiona hapati anachotaka haraka, ataenda pengine ambapo ataweza kupata kile anachotaka haraka.

Hivyo kwa kujua hili, unahitaji kufanya marekebisho kwenye biashara yako, ili kuweza kuwahudumia vizuri wateja na kuendelea kuwa nao. Hakikisha unakuwa na rasilimali za kutosha kuwahudumia wateja kwa wakati. Jua kabisa muda wa mteja kusubiri mpaka apate huduma kwako ni kiasi gani, na punguza muda huo ili kuweza kuwahudumia wateja wengi zaidi.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanakosa wateja kwa sababu wamekuwa hawajali muda wa wateja wao. Wamekuwa wanafikiri wateja watakuja na watasubiri kwa sababu wana shida. Wanasahau kwamba wapo wengi wanaoweza kutatua shida hiyo.

Watu hawana subira kabisa katika zama hizi, epuka kuwasubirisha watu kwenye biashara yako kwa sababu zisizo za msingi. Weka vizuri rasilimali zako ili kuwapa wateja huduma bora na kwa wakati.

Hizi ni zama za kasi, watu wanatukuza chochote chenye kasi. Hakikisha biashara yako inatoa huduma na bidhaa kwa kasi ambayo itawaridhisha wateja wako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.