UKURASA WA 798; Njia Mbili Za Kuongeza Faida Na Moja Ya Kuepuka Sana….

By | March 8, 2017

Zipo sababu nyingi zinazopelekea watu kuanza biashara au kujiajiri, lakini biashara zote ili ziweze kuendelea, lazima zitengeneze faida. Bila ya faida biashara hata iwe nzuri na ya msaada kiasi gani kwa wateja wake, itakufa.

IMG-20170228-WA0004

Hivyo kama mfanyabiashara lazima uweke jicho lako kwenye faida, ujue unaelekea wapi kwa rasilimali unazoweka kwenye biashara yako. Kadiri faida inavyokuwa kubwa, ndiyo biashara pia inavyopata nafasi ya kukua.

Kwa sababu hii, wafanyabiashara wengi, wamekuwa wakikazana kukuza faida za biashara zao. Na zipo njia nyingi sana za kuweza kukuza faida ya biashara yoyote ile. Ila njia hizi zimegawanyika kwenye makundi makuu mawili.

Kundi la kwanza ni kuongeza thamani zaidi kwa wateja wa biashara yako. Kuongeza vitu ambavyo vitawafanya wateja kulipia zaidi na hata kuongeza wateja wapya zaidi. Hapa unahitaji kuwa na ubunifu na kuwajua wateja wako vizuri ili kuweza kuwapa kile ambacho kitayafanya maisha yao kuwa bora zaidi. Ukishayajua matatizo na mahitaji ya wateja wako, utaweza kujua njia za kuongeza thamani kwako.

SOMA; Mshahara Au Faida Pekee Haitakufikisha Kwenye Utajiri.

Kundi la pili ni kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara yako. Hapa unahakikisha gharama kwako zinakuwa chini kabisa, bila ya kujali mteja anapata huduma bora au la. Hivyo unaweza kupunguza vitu vingi, mfano kupunguza wafanyakazi, kuajiri wafanyakazi wenye uwezo mdogo ili kuwalipa kidogo, kupunguza bajeti ya kutangaza biashara na vitu vingine vya aina hiyo. Kwa njia hii unahakikisha unaweza kwenda na biashara kwa gharama za chini kabisa.

Katika makundi haya mawili, kundi la kwanza ni gumu kufanya, kwa sababu hapo unahitaji ubunifu, na pia unahitaji muda kuweza kutengeneza thamani kwenye maisha yako. Lakini pia ni njia bora sana kufuata kwa sababu unapoongeza thamani kwa wateja wako unakuza biashara yako zaidi.

Kundi la pili ni rahisi kufanya, kupunguza tu gharama, unaweza kuondoa chochote unachoweza kufikiria kuondoa, ili kupunguza gharama. Lakini ni njia hatari sana kwa sababu unazidi kudidimiza biashara yako. Unatoa huduma mbovu, unaondoa bajeti muhimu na biashara inaelekea kufa.

Hivyo kwako wewe rafiki yangu, kila unapofikiria kuongeza faida kwenye biashara yako, fikiria ni thamani gani unayoweza kuongeza kwa wateja wako. Kwa kufikiri hivi, utaziona njia nyingi za kuongeza faida na hata kukuza biashara yako zaidi.

Usitumie njia ya pili, hiyo ni njia ya kuelekea kwenye kifo, ni njia hatari sana kwa maendeleo ya biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.