UKURASA WA 806; Nikiwa Tayari Nitakutafuta…

By | March 16, 2017

Ni mara ngapi umesikia kauli kama hiyo?

Labda ni mteja ulikuwa unamweleza kuhusu bidhaa au huduma ambayo unatoa, umetumia muda wako kumweleza vizuri, na mwisho akakupa kauli hiyo?

IMG-20170306-WA0004

Au labda ni kazi ulienda kuomba mahali, ukafanyiwa usaili vizuri na kila kitu kikakamilika, lakini mwisho wakakupa kauli hiyo?

Au ni mipango ulikuwa umepanga na mtu, labda ya kuanza kitu pamoja, au akusaidie kitu fulani ambacho ni muhimu kwako, mwisho anakupa kauli hiyo.

Nina uhakika, umeambiwa kauli hiyo mara nyingi mno, na kutoka kwa watu mbalimbali, kwenye kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla.

Swali langu la pili ni hili, ni wangapi kati ya hao waliokuambia wakiwa tayari watakutafuta, walikutafuta kweli? Ni wangapi kati ya wateja waliokuambia watakutafuta walikuja kukutafuta kweli? Vipi kwenye kazi na hata ahadi nyingine kwenye maisha?

Kwa wengi, ni mara chache sana watu wale wanakuja kukutafuta kweli, na kati ya wengi wanaosema watakutafuta, ni wachache ndiyo wanafanya hivyo. Wengi hawakutafuti, na mbaya zaidi, ukija hata kuwakumbusha vipi ulisema utanitafuta, watakuuliza kukutafuta kwa nini? Wameshasahau kabisa hata mlikuwa mnazungumzia nini mpaka akasema atakutafuta. Kwa sababu huenda ameshawaambia wengi neno hilo.

SOMA; Dalili Saba Kwamba Tayari Wewe Una Mtizamo Chanya Utakaokufikisha Kwenye Mafanikio Makubwa.

Nikiwa tayari nitakutafuta ni njia ya kistaarabu ya kukuambia kwamba sitaki, au sitaweza kufanya. Watu wengi hawapendi kuwavunja wengine moyo, na hivyo huepuka kutumia maneno makali ambayo yatawakatisha tamaa. Badala yake wanatafuta maneno mazuri ambayo yatamfanya mtu ajisikie vizuri. Na moja ya maneno hayo ni hili… nikiwa tayari nitakutafuta….

Hivyo mtu anapokuambia nikiwa tayari nitakutafuta, usifurahie tu na kukubali haraka, bali endelea kumhoji kuhusu utayari wake. Unaweza kumuuliza kwa sasa hayupo tayari kwenye jambo gani na nini kinamzuia asichukue hatua sasa hivi. Kama ana sababu ya kweli atakueleza, kama hana sababu atababaika babaika na utajua alikuwa anakuambia kukuridhisha tu.

Mwisho kabisa mwulize umkumbushe lini? Ni siku gani hasa umkumbushe kuhusu ahadi yake ya kukutafuta, asikuambie tu baada ya wiki mbili, au baada ya mwezi, bali akuambie siku kabisa. Kwa mfano akikuambia baada ya mwezi, unaweza kumwuliza kwa hiyo nikutafute alhamisi ya tarehe 13? Huku ukiandika tarehe hiyo. Kama kweli anamaanisha atakuambia ndiyo, kama alikuwa anakuridhisha utamwona anababaika. Na hapo utajua hatua ipi sahihi ya kuchukua.

Kumbuka unapouliza maswali haya usiulize kwa ukali au kwa kuonesha huna imani na alichokuambia, bali uliza ukionesha kwamba unajali sana kile alichokuambia. Na pia usiulize kwa ukali kama mahojiano ya polisi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.