UKURASA WA 820; Aina Mbili Za Wateja Wa Biashara Yako…

By | March 30, 2017

Biashara ni wateja, na dhumuni kuu la biashara ni kutengeneza wateja watakaokuwa waaminifu kwenye biashara yako. Faida ni zao la uwepo wa wateja kwenye biashara, mzunguko wa fedha ni matokeo ya mauzo yanayotokea iwapo biashara ina wateja.

IMG-20170316-WA0010

Zipo aina mbili za wateja wa biashara yako, ambazo unapaswa kuzijua ili kuweza kuongeza zaidi wateja wa biashara yako.

Aina ya kwanza ni wale wateja ambao kila siku wapo, wanakuja kununua au kupata huduma unazotoa kwenye biashara yako. Wanaweza kuwepo kwa sababu kuna thamani wanayoipata, au wanakuwepo tu kwa sababu wameshazoea. Kwenye biashara yoyote ile wapo wateja ambao wapo siku zote. Hawa ni wateja muhimu ambao unahitaji kuwapa thamani kwa kuwahudumia vizuri, kwa sababu hawa ndiyo watakaokuletea wateja wa aina ya pili.

Aina ya pili ni wale wateja ambao wanaambiwa hebu mcheki fulani, hebu nenda sehemu fulani. Hawa ni wateja ambao kuna kitu wanatafuta, halafu wanaambiwa wanaweza kukipata kwako. Au wana shida fulani na wakaambiwa wakija kwako watatatuliwa shida yao. Hawa ni wateja ambao unahitaji kuwapa huduma nzuri pia ili kesho na keshokutwa waje tena. Wanapojaribu siku ya kwanza na wakapata kweli kile walichotaka, wanakuwa wateja wako kila siku, na huenda wakaleta wengine zaidi.

SOMA; Cross-Selling Na Up-Selling, Mbinu Mbili Za Kuongeza Mauzo Bila Kuongeza Wateja.

Sasa kikubwa sana ninachotaka uelewe ni hichi, wanaofanya biashara kama unayofanya wewe ni wengi sana. Kitakachomfanya mtu amwambie mwingine mcheki huyu au nenda pale, ni kama umejiweka kama mtu anayetoa suluhisho kwa changamoto fulani au umekuwa unatoa huduma bora sana.

Hivyo unapotoa huduma kwa wateja wako wa sasa, usiwaangalie tu wao, bali angalia kwa huduma unazowapa, je wapo tayari kuwaambia wengine wengi kuhusu biashara yako? Kama jibu ni ndiyo basi upo pazuri. Kama jibu ni hapana fanyia kazi kile ambacho siyo sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.