UKURASA WA 821; Maliza Unachoanza….

By | March 31, 2017

Hakuna kitu kinapoteza muda kwenye maisha yetu, kama kuanza kitu halafu humalizi. Unakuwa umeweka muda na rasilimali nyingine, halafu unaishia njiani, humalizi. Unakuwa umewekeza lakini hujapata manufaa kamili. Sawa na mwindaji ambaye amekwenda kuwinda, kamwona swala, akamchoma mkuki, swala akaendelea kukimbia, lakini sasa kwa kasi ndogo, ila mwindaji akaamua kuachana naye. Hapo haina msaada kwa swala wala kwa mwindaji.

IMG-20170303-WA0002

Unapoanza kufanya kitu maana yake unafungua ukurasa mpya kwenye akili yako, mawazo yako na hata maisha yako kwa ujumla. Unapoishia njiani bila kukamilisha, kitu kile kinaendelea kushika nafasi kwenye akili yako, mawazo yako na hata maisha yako kwa ujumla.

Unakuwa kama mzigo ambao unakuchosha lakini huutui, unaendelea kuubeba tu mpaka mwisho. Inakuzuia hata kuanza jambo jipya na muhimu zaidi. Kwa sababu kila wakati unajiona una mambo mengi ya kufanya, unajiona upo bize na huna muda. Kumbe umekusanya mengi ambayo hujayakamilisha.

Ili kuondokana na hali hii, kuna mambo muhimu mawili ya kufanya.

Kwanza hakikisha unaweka vigezo muhimu vya yale ambayo upo tayari kufanya. Usikimbilie tu kuanza kufanya kila kitu, hakikisha unachofanya unakithamini kweli na kinastahili muda na nguvu zako. Usiwe na haraka ya kufanya kila kitu, jua muda ni rasilimali adimu kwako.

SOMA; Bila Kuwajua Watu Hawa Watatu Na Kumalizana Nao, Sahau Kuhusu Mafanikio.

Pili maliza kila unachoanza, ukishaweka vigezo na kitu kikakidhi vigezo vyako na ukakianza, basi usikubali kuishia njiani. Usikubali hata kidogo, hakikisha unakwenda mpaka mwisho, hakikisha unakamilisha unachoanza.

Chochote ambacho una thamini kukifanya, basi kifanye mpaka mwisho. Kama huwezi kukifanya mpaka mwisho, ni bora usikianze kabisa, kwa sababu haitakuwa na msaada kwa yeyote. Ni sawa na mwindaji anayemchoma swala mshale na kumwacha aende zake, hapati kitoweo na maisha ya swala kayaharibu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.