UKURASA WA 827; Nidhamu Binafsi Siyo Kujitesa…

By | April 6, 2017

Ukiniuliza ni kitu gani kimoja ambacho watu wanaokazana sana kwenye maisha lakini hawapigi hatua wanakikosa, sitasita hata kidogo, nitakuambia ni NIDHAMU BINAFSI.

IMG-20170228-WA0007

Watu wengi wanajua kila wanachopaswa kujua ili kufanikiwa. Wanazijua vizuri hadithi za watu walioanzia chini na wakapambana mpaka wamefika juu. Wanajua kila mbinu za kuanzisha na kukuza biashara. Lakini mbona hawatumii hayo wanayojua ili kufanikiwa?

Jibu ni rahisi, wamekosa nidhamu binafsi. Hawana uvumilivu wa kutosha kuweza kufanya kitu sasa hivi, ambacho hakina matokeo ya haraka. Hawawezi kupanga kitu na kukifanya kama walivyopanga. Watapanga mengi sana lakini inapofika hatua ya utekelezaji, sababu zinaingilia kati, na kwa kuwa hawana nidhamu binafsi, hawawezi kuzishinda hizo sababu.

Unahitaji nidhamu binafsi ili kuweza kuamka asubuhi na mapema kila siku.

Unahitaji nidhamu binafsi ili uweze kuandika kila siku.

Unahitaji nidhamu binafsi ili uweze kujilipa wewe mwenyewe angalau sehemu ya kumi ya kipato chako.

Unahitaji nidhamu binafsi ili uweze kuwekeza.

Unahitaji nidhamu binafsi ili uweze kukataa raha ya muda mfupi ambayo haidumu, na kusubiri furaha ya muda mrefu ambayo itakuchukua muda kuifikia.

SOMA; Nidhamu Ndio Nguzo, Ukiikosa Utaanguka.

Kwa nini nidhamu binafsi inakuwa shida?

Nidhamu binafsi inakuwa shida kwa wengi kwa sababu wanachukulia nidhamu binafsi kama kujitesa. Pale inapombidi mtu kuacha kile anachokiona ni kizuri kwa sasa, na kufanya kazi ili kutengeneza kikubwa zaidi cha baadaye, anachukulia kwamba anajitesa.

Pale mtu anapokatisha usingizi kwa ajili ya kuamka mapema na kufanya shughuli zake muhimu, anaona kama anajitesa.

Pale mtu anapoacha kununua vitu vya kuonekana, kama wengine wanavyofanya, badala yake akajilipa fedha hiyo na kuwekeza, anaona kama anajinyima.

Sasa ukishaanza na mtazamo huu wa kujinyima, huwezi kupiga hatua. Maana utaona unajitesa, utaona hujitendei haki na hatimaye utaacha kufanya yale muhimu kwa mafanikio na kuishia kufanya yale ya muda mfupi.

Nidhamu binafsi siyo mateso, nidhamu binafsi siyo kujinyima, nidhamu binafsi siyo kuzika kabisa mahitaji yako, bali nidhamu binafsi ni pale unaacha mahitaji yako makubwa ya mafanikio, yachukue nafasi ya mahitaji yako madogo ya raha za muda mfupi.

Pale unapoweza kuacha kitu kinachokupa raha sasa na raha ya muda mfupi, na kufanya kile ambacho hakina raha sasa, lakini baadaye kitakuletea mafanikio makubwa.

Huu ndiyo mtazamo sahihi wa nidhamu binafsi, ambao ukienda nao utaweza kujijengea vizuri nidhamu binafsi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.