UKURASA WA 833; Kanuni Moja Ya Maajabu Ya Mafanikio Kwenye Biashara…

By | April 12, 2017

Haipo, watu wanapenda kusikia kanuni moja ya maajabu, yaani kitu kimoja tu ambacho ukikifanya biashara yako itafanikiwa sana. Ukitaka uwapate wengi zaidi sema siri, maana pia watu wanaamini zipo siri ambazo wao hawazijui ila wengine ndiyo wanazijua. Pia hakuna siri, siri ni kile usichokijua wewe, ambacho hakijafichwa popote, ila wewe tu hujataka kukitafuta.

IMG-20170321-WA0000

Hivyo basi, kufanikiwa kwenye biashara, kama ilivyo kwenye maisha, lazima ufanye kila kitu, KILA KITU. Lazima ujue kila kitu kuhusu biashara, kuhusu fedha, kuhusu uchumi, kuhusu watu, kuhusu saikolojia na mengine mengi. Ndiyo maana huwa nasema biashara ni chuo kikuu cha maisha, utajifunza mengi sana kila siku.

Lakini wengi wanapoingia kwenye biashara, wanaingia na mtazamo wa kununua na kuuza, ndiyo maana hawapigi hatua kubwa zaidi ya kununua na kuuza. Wanapojaribu kufanya mengine kwa mazoea kama wanavyonunua na kuuza, wanakutana na changamoto kubwa na kuona mambo hayawezekani.

SOMA; Kanuni Rahisi Ya Furaha…

Wito wangu kwako leo rafiki yangu ni huu, acha kukimbiza njia moja ya uhakika, acha kukimbizana na siri, acha kutafuta kanuni ya maajabu na badala yake, tumia muda wako kuijua vizuri biashara yako na kujua kila kitu kinachoihusu biashara yako.

Kila eneo la biashara yako linalokupa changamoto, kaa chini na jifunze ni hatua zipi za kuchukua. Labda unaajiri watu na wanakusumbua, kaa chini na ujifunze kuhusu tabia za watu, saikolojia za watu, namna ya kuwashawishi watu na maarifa mengine muhimu kuhusu watu. Ukishawajua watu vizuri utaweza kutatua changamoto mbalimbali unazozipata kuhusu watu kwenye biashara yako.

Kadhalika kwenye mzunguko wa fedha, jua kila kitu kuhusu mzunguko wa fedha kwenye biashara yako na hata kwenye uchumi kwa ujumla. Kadiri unavyokuwa na maarifa sahihi, inakuwa rahisi kwako kufanya maamuzi sahihi.

Jua kila kitu, fanya kila kitu kwenye biashara yako. Hakuna mwingine atakayejua na kufanya zaidi yako, ni biashara yako, wengine watafanya kama unavyofanya wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.