UKURASA WA 839; Haijalishi Hali Ya Uchumi Ikoje, Fursa Za Kutengeneza Fedha Bado Ni Nyingi…

By | April 18, 2017

Popote ambapo watu wapo, ipo fursa ya kutengeneza fedha, bila ya kujali hali ya uchumi ni ngumu kiasi gani, bila ya kujali thamani ya fedha imepanda au kushuka kiasi gani.

IMG-20170406-WA0013

Popote penye watu pana fursa kwa sababu watu wana matatizo, na yeyote awezaye kuwatatulia watu matatizo yao na kuwapa kile ambacho wanakitaka, kwa namna bora zaidi ya wanavyopata sasa, ana nafasi kubwa ya kutengeneza kipato kikubwa.

Matatizo ya watu huwa hayaishi, na hata yale ambayo yalishatatuliwa bado yanahitaji kuboreshwa zaidi na zaidi, ndiyo maana wanaojua kutatua matatizo huwa hawaishiwi na fursa.

Kwa mfano, hata iweje, watu lazima wale, halina ubishi hilo. Hivyo chakula kitaendelea kuwa fursa, na hata kama chakula kitakuwa kinapatikana kwa wingi, litakuwepo hitaji la chakula bora zaidi kwa afya, hivyo fursa hazitakauka kwenye eneo la chakula.

Watu lazima wavae, hakuna watakaotembea uchi hata mambo yawe magumu kiasi gani. Hivyo hata kama hawataweza kugharamia kiasi kikubwa kuvaa, watakuwa tayari kugharamia mavazi bora wanayoweza kumudu.

SOMA; Kanuni Moja Ya Maajabu Ya Mafanikio Kwenye Biashara…

Watu lazima watoke eneo moja kwenda jingine, kwa usafiri wao binafsi au usafiri wa umma. Hata mambo yawe magumu kiasi gani, watu hawataweza kuendelea kubaki sehemu moja bila ya kusafiri iwe ni safari fupi au ndefu.

Hivyo rafiki, ninachotaka kukuambia hapa ni kwamba, wakati watu wanalalamika uchumi ni mgumu au mambo hayaendi, wewe kazana kuangalia ni namna gani ambavyo unaweza kutatua matatizo ya watu. Na ukiweza hili, fedha hazitakauka kwako. Angalia matatizo ya watu na yatatue, hivyo ndivyo utakavyoweza kutengeneza fedha kwenye zama hizi.

Shida inakuja kwa wale wanaotaka mambo marahisi, wanaofanya kwa mazoea na wanaotegemea wengine kupewa kipato. Hawa lazima uchumi uwaumize sana mpaka pale watakapokubali kutumia akili zao vizuri.

Kampuni ya pikipiki ya honda ilianza hivi hivi, mmiliki wake alikuwa anatengeneza vifaa vya magari ya toyota. Hali ya uchumi ikawa ngumu na toyota wakawa hawanunui tena vifaa vyake. Akakosa hata fedha ya kuweka mafuta kwenye gari yake, ndipo akafikiria kutafuta njia rahisi ya kusafiri, akapata wazo la kufunga injini ndogo kwenye baiskeli. Alifanikiwa na kila alipopita mtaani, watu walimwambia awatengenezee na wao pia. Na hapo ndipo alipoanza kutengeneza pikipiki kwa ajili ya wengi.

Leo na kila siku, unaposikia mtu anasema uchumi mgumu, fedha hakuna, au wazo hili likakujia wewe, haraka sana andika mahali ni matatizo gani unaona wengine wanayo. Au ni matatizo gani wewe mwenyewe unayo, anza kuyatatua na wapo wengi kama wewe ambao ukiwawezesha kutatua watakuwa tayari kukulipa.

Tatua matatizo ya watu, hiyo ndiyo fursa isiyoisha ya kutengeneza fedha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.