UKURASA WA 840; Chochote Usichokijua Ni Kigumu…

By | April 19, 2017

Huwa nawahoji sana watu ambao wana malengo na ndoto kubwa, lakini hawajachukua hatua yoyote ili kuweza kufikia malengo na ndoto hizo. Na swali langu kubwa huwa ni kwa nini mpaka sasa hujafika pale unapotaka kufika, au kwa nini mpaka sasa hujaanza. Na majibu yote huwa yanaelekea sehemu moja, ni vigumu kufanya.

IMG-20170218-WA0000

Lakini kile ambacho watu wanasema ni kigumu, wapo wengine wanakifanya bila shida yoyote. Pale watu wanasema hawana mtaji wa kuanza biashara, wapo watu wameanza biashara bila ya mtaji wowote. Pale watu wanasema biashara ni ngumu au hailipi, wapo watu wanaifanya vizuri na kufanikiwa sana.

Hivyo nimekuwa na wasiwasi juu ya ugumu, je upo kwa wachache tu au unachagua watu? Lakini nimepata jibu moja, ugumu wowote upo mwanzoni. Kitu chochote ambacho mtu hajawahi kukifanya, kinakuwa kigumu sana kwake. Akifikiria mambo yote ya kufanya mpaka afike kule anakotaka kufika, anajikuta anakata tamaa na kuona hawezi.

Sasa ili kuondokana na ugumu huu, hasa huu wa mwanzo, ninakupa njia moja nzuri. Usiangalie zaidi kule unakotaka kufika na kufikiria unafikaje pale, bali panga ni vitu gani unahitaji kufanya kila siku, ambavyo vitakufikisha pale. Halafu fanya vitu hivi, sahau hayo makubwa mengine. Utakaporudia kufanya vitu hivi kila siku, vinakuwa rahisi kwako na utaweza kuboresha zaidi na zaidi.

SOMA; Wasaidie Kuondokana Na Hofu Ya Kutokujua…

Kwa mfano kama biashara ni ngumu kwako kuanza, angalia hatua ipi ya kuanzia. Kuwa na huduma au bidhaa ambayo mteja anaihitaji, kumtafuta mteja anayeihitaji na kumuuzia. Hivyo basi, jukumu lako kuu ni kuwa na kile mteja anahitaji, halafu kumfikia mteja na kumuuzia. Hii ni hatua ya msingi ya kuanzia na anza na hii kila siku. Baadaye ndiyo unaweza kujali kuhusu mengine, baada ya kuwa na mteja na akawa amenunua.

Chochote unachokiona kigumu, kigawe kwenye magungu madogo madogo ambayo unaweza kuyafanyia kazi kila siku.

Hata kama unataka kuandika kitabu, usiangalie kitabu kama kitabu, bali angalia kila siku unaweza kuandika nini. Andaa sura zako za kitabu na kila siku jipe wajibu wa kuandika maneno 500 tu, au hata 1000 tu na baada ya mwezi mmoja, unaweza kuwa na kitabu chako tayari.

Kitu kigumu ni kile ambacho hujakifanya, anza kufanya na ugumu unapotea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.