UKURASA WA 843; Chimbuko La Matatizo Yote Ya Binadamu….

By | April 22, 2017

Charles Munger, bilionea mwekezaji, amewahi kunukuliwa akisema kwamba matatizo yote ya binadamu chimbuko lake ni mtu kushindwa kukaa kwa utulivu akiwa ndani ya chumba peke yake. Alikuwa akishauri kuhusu uwekezaji na kusema kwamba siri kuu ya mafanikio kwenye uwekezaji ni utulivu na uvumilivu. Na hilo ndilo ambalo wengi huwa hawawezi kufanya.

IMG-20170322-WA0009

Nimejaribu kulifikiria hilo kwenye kila eneo la maisha yetu, na naona kweli kushindwa kutulia ni chimbuko la matatizo mengi, hasa pale tunapokuwa peke yetu, au tunapokuwa wapweke.

Binadamu hatupendi kabisa kuwa wapweke, hivyo tunapokuwa wenyewe, tunatafuta kila namna ya kuondokana na upweke wetu. Tutatafuta nani wa kwenda kuongea naye, au kuangalia tv, kusikiliza redio, na kwa dunia ya sasa, kuperuzi mitandao ya kijamii bila kikomo. Wengine wanakwenda mbali zaidi na kutumia vilevi kama pombe na hata madawa ya kulevya.

SOMA; Nani Atarithi Matatizo Na Changamoto Zako?

Vita yako kuu ni kuweza kuondokana na hali hiyo, kuweza kukaa ukiwa umetulia ndani ya chumba peke yako, bila ya kukimbilia kushika simu, wala kuanza kuangalia nani wa kuongea naye. Kaa ukiwa umetulia na tafakari maisha, angalia ndoto zako na angalia hatua unazochukua.

Kujikomaza kwenye hili, kila siku jipe muda maalumu ambao utakuwa wewe peke yako, bila ya mtu, bila ya simu, na bila ya kilevi. Ni wewe ukiyasikiliza mawazo yako na kutafakari kwa kina. Ukizoea kufanya hivi, utaweza kutatua matatizo mengi sana yanayokusumbua.

Watu wengi wamekuwa wakiruka ruka, yote hayo kukwepa kukaa chini na kufikiri kwa kina. Usiwe mmoja wa watu hao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.